Baba Mtakatifu Francisko, amepokea kwa masikitiko makubwa habari za kifo cha Padre
Gregorio Lòpez Gorostieta aliyeuwawa hivi karibuni huko Mexico. Katika ujumbe ulioandikwa
kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu
Maximino Martines Miranda, wa Jimbo Ciudad Altamirano, anapenda kutoa salam zake za
rambi rambi kwa wote walioguswa na msiba huu wa kutisha na kwamba, anawakumbuka na
kuwaombea katika sala zake.
Baba Mtakatifu anasema, haya ni mauji ya mtu asiyekuwa
na hatia na wala hayana msingi wowote. Baba Mtakatifu anatumia fursa hii kulaani mauaji,
nyanyaso na dhuluma dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu anawahamasisha
Wamissionari Jimboni humo kusonga mbele kwa imani na matumaini bila kuogopa wala kukata
tamaa licha ya magumu na changamoto wanazokabiliana nazo, huku wakifuata mfano wa
Yesu Kristo mchungaji mwema. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha mshikamano wake wa karibu
kwa wazazi, ndugu na jamaa ya Marehemu Padre Gorostieta.