2014-12-31 10:30:25

Mwaka wa Bwana uliokubalika!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini, linawatakia waamini na wananchi wote wa Ufilippini, kheri, baraka na amani kwa mwaka 2015, ili kweli uwe ni Mwaka wa Bwana, unaosheheni matukio makubwa ya kiimani. Mwaka 2015 ni Mwaka wa Watawa Duniani, ni Mwaka wa Maskini nchini Ufilippini ni Mwaka ambao, Baba Mtakatifu Francisko anatembelea nchini Ufilippini, ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, upendo na huruma.

Askofu mkuu Socrates Villegas, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini katika ujumbe wake kwa Mwaka Mpya wa 2015, anawataka waamini kwa namna ya pekee kabisa kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano na jirani zao, ili kweli Mwaka 2015 uwe ni Mwaka wa Bwana uliokubalika, ili kumtukuza, kumshukuru, kumwomba na kumwabudu Mwenyezi Mungu.

Uwe ni mwaka ambao, waamini wanajitahidi kila siku ya maisha yao, kuupamba kwa njia ya upendo kwa Mungu na jirani; uweni mwaka ambao, waamini wanaweza kukabiliana na changamoto na magumu ya maisha kwa njia ya imani thabiti bila kuyumba; uwe ni mwaka ambao waamini wanaonesha imani tendaji kwa Kristo na Kanisa lake, huku wakijitahidi kuwashirikisha wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku. Mwaka 2015, uwe kweli mwaka imani, matumaini na mapendo.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linakumbusha kwamba, Mama Kanisa ameutangaza Mwaka 2015 kuwa ni Mwaka wa Watawa Duniani, changamoto na mwaliko kwa Familia ya Mungu kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya zawadi ya maisha ya kuwekwa wakfu ndani ya Kanisa. Maisha yao yanayojikita katika Mashauri ya Kiinjili, yaani: Ufukara, Utii na Useja, yawe ni kielelezo cha uwepo endelevu wa Mungu kati ya watu wake hapa duniani.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini limeutangaza Mwaka 2015 kuwa ni Mwaka wa Maskini, kama sehemu ya mchakato wa Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 500 ya Uinjilishaji nchini Ufilippini, ambao utafikia kilele chake kunako mwaka 2021. Katika kipindi cha mwaka mzima, Kanisa Katoliki Nchini Ufilippini linaadhimisha mwaka huu kwa matukio mbali mbali yanayofanyika kwa ngazi ya Kiparokia, Kijimbo na Kitaifa, ili kuhakikisha kwamba, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wanapata kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa.

Ni mchakato unaopania pamoja na mambo mengine kuwajengea uwezo maskini, ili waweze kushiriki katika mikakati ya kujiletea maendeleo yao endelevu. Maaskofu wanakumbusha kwamba, maskini ni sura ya Kristo mhitaji na kwamba, katika umaskini wao, Yesu Kristo mwenyewe anakuwa ni hazina yao!

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linasema, Mwaka 2015 kwao ni Mwaka wa baraka na neema nyingi kwani wanasubiri kwa imani na matumaini, ujio wa Baba Mtakatifu Francisko anayetembelea Sri Lanka na hatimaye, nchini Ufilippini. Ni wakati wa neema, imani na matumaini mapya kwa waamini na wananchi wote wa Ufilippini, kwani Baba Mtakatifu anataka kuwaimarisha katika imani, huruma na mapendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.All the contents on this site are copyrighted ©.