2014-12-31 10:35:58

Kuta za utengano na Mapazia ya chuma yametoweka, lakini...!


Mheshimiwa Martin Junge, Katibu mkuu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani anasema, inafurahisha sana kusikia kwamba, kuna bahari ya vijana kutoka Barani Ulaya wanaokutanika mjini Prague, Jamhuri ya Watu wa Czech, ili kusali, kutafakari na kusikiliza kwa makini Neno la Mungu. Kwa njia hii moto wa imani unaendelea kuwashwa na kuimarisha upendo katika shida na mahangaiko mbali mbali.

Ni tukio ambalo linafanyika nchini Czech wakati huu inapoadhimisha Jubilee ya miaka ishirini na mitano tangu demokrasia ya kweli iliporejea tena nchini humo. Ni jambo ambalo lisingewezekana kufikirika au kutendeka katika kipindi cha miaka thelathini iliyopita. Kuta na mapazia ya chuma yaliyojengwa ili kuwatenganisha watu, yameporomoka; amani na usalama wa kufikirika, vimetoweka na watu wanaonesha upendo wa kweli Huu ndio mchakato wa kweli wa mabadiliko ulioleta mapinduzi Barani Ulaya.

Vijana wamechangia kuhakikisha kwamba, kuta na mapazia ya chuma yanatoweka miongoni mwa watu kwani walitambua kwamba wao ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa; chachu ya haki, amani na upatanisho katika ulimwenguni unaosheheni madonda ya utengano na mgawanyiko.

Katibu mkuu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani anasema kwamba, kuta za utengano zimesogezwa kwenye mipaka ya Bara la Ulaya, kama kizuizi kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama na maisha bora. Ni kundi la watu linalotafuta fursa za ajira; watu ambao wamekimbia nchi zao kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kwa hakika athari za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya changamoto kubwa zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa, changamoto kwa wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanaivalia njuga changamoto hii.

Vijana wanahamasishwa kujikita katika mchakato wa upatanisho ambao ni hija inayoendelea kuwashangaza wengi na kuwataka kujisadaka kikamilifu katika dhamana hii kwa kupenda, ili hatimaye, kuleta mabadiliko katika ulimwengu mamboleo. Jumuiya ya kiekumene ya Vijana wa Taizè, tangu tarehe 29 Desemba hadi tarehe 2 Januari 2015 wamekuwa wakisali na kutafakari Neno la Mungu, tayari kuwatangazia Watu wa Mataifa ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.All the contents on this site are copyrighted ©.