Jamani, tegeni sikio msikilize kile anachosema Papa Francisko!
Juhudi zinazofanywa na Baba Mtakatifu Francisko katika kulinda, kutetea na kuendeleza
utu na heshima ya binadamu; haki na amani; ustawi na maendeleo ya wengi zinapaswa
kuungwa mkono na watu wote wenye mapenzi mema sehemu mbali mbali za dunia, lakini
kwa namna ya pekee na wananchi wa Ufilippini ambao wanasubiri kwa hamu kubwa, ujio
wa Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao!
Ni mwaliko maalum unaotolewa na Alhaji
Ebra M. Moxsir, Kiongozi mkuu wa Baraza la Maimamu wa dini ya Kiislam nchini Ufilippini
anayewaalika ndugu zake Waislam pamoja na watu wenye mapenzi mema, kumsikiliza kwa
makini ushauri unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko ili kushinda vitendo vya kigaidi,
kwa kujenga na kuendeleza majadiliano ya kidini, ili kupata amani ya kweli na inayodumu.
Alhaji
Moxsir ameyasema haya katika mahojiano maalum na Kituo kimoja cha Televisheni nchini
Ufilippini, kwa kukazia mahusiano mema ya kidini miongoni mwa waamini wa dini mbali
mbali, mahusiano yanayojikita katika misingi ya: ukweli, uwazi, upendo, mshikamano
na mafao ya wengi. Kuna haja ya kuondokana na misimamo mikali ya kiimani inayohatarisha
usalama na maisha ya watu na hivyo kuwa kikwazo kikuu cha maendeleo na ustawi wa watu.
Waamini wafundishwe kanuni msingi za imani yao, ili kuishuhudia katika uhalisia wa
maisha ya kila siku. Misimamo mikali ya kidini ni matokeo ya waamini kutofundwa kikamilifu
katika misingi ya imani na kanuni maadili.
Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu
Francisko anatarajiwa kufanya hija yake ya kichungaji Barani Asia kuanzia tarehe 12
hadi tarehe 19 Januari 2015. Akiwa nchini Ufilippini, Baba Mtakatifu atakutana na
kuzungumza na wahanga wa tufani ya Yolanda, iliyopelekea maafa makubwa kwa watu na
mali zao. Anatarajiwa pia ukutana na kuzungumza na viongozi wa kidini, ili kuimarisha
mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya
watu: kiroho na kimwili.
Kwa maneno mengine, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu
Francisko nchini Ufilippini inapania kuwatia moyo waamini ili kujikita zaidi katika
mchakato wa kupambana na umaskini kwa njia ya huduma inayosimikwa katika upendo na
huruma! Vijana wengi kutoka Ufilippini wanaendelea kujiandaa ili kukutana na kuzungumza
na Baba Mtakatifu Francisko, ili aweze kuwatia shime katika mchakato wa Uinjilishaji
mpya. Tukio la vijana kukutana na Baba Mtakatifu Francisko, litapambwa kwa sala, tafakari
na Ibada ya Rozari Takatifu. Vijana wanatarajiwa kutoa ushuhuda wa imani yao kwa Kristo
na Kanisa lake!