2014-12-31 10:18:50

Haki inapokosekana, amani na utulivu viko mashakani!


Askofu Renatus Nkwande wa Jimbo Katoliki Bunda, Tanzania, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, ikiwa kama watu wanataka kudumisha amani ya kweli wanapaswa kutendeana haki kama sehemu ya utekelezaji wa kanuni ya dhahabu! RealAudioMP3

Askofu Nkwande anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2015 anaorodhesha mambo msingi ambayo yamekuwa ni sababu ya kutoweka kwa amani duniani. Anasema, utumwa mamboleo na biashara haramu ya binadamu ni mambo ambayo yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu; huu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko.

Rushwa na ufisadi ni mambo ambayo yanatembezwa nje nje tu kana kwamba hakuna maadili wala sheria. Kuna nyanyaso za watoto wadogo na mauaji ya wazee na watu wenye ulemavu wa ngozi. Mambo yote haya anasema Askofu Nkwande msingi wake ni dhambi ya ubinafsi inayomplekea mtu kushindwa kutambua utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Pale haki inapokesekana na mwanadamu anaposhindwa kumwogopa Mwenyezi Mungu, amani na utulivu viko mashakani.

Askofu Nkwande anasema, ili kudumisha haki, amani na utulivu kuna haja kwa watu kujifunza kutenda haki, tangu wakiwa katika umri mdogo. Watu wajitahidi kushuhudia kwamba, haki na amani ni mambo yanayowezekana katika maisha ya mwanadamu, ikiwa kama watu watapania kumwilisha haki maishani mwao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.All the contents on this site are copyrighted ©.