2014-12-31 11:55:19

Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa!


Katika sikukuu ya Noeli tuliadhimisha utukufu wa Mungu katika kuzaliwa kwake kama mwanadamu, utukufu unaojionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Umwilisho! Leo – tunaadhimisha matokeo ya kuzaliwa kwake kwetu. Bikira Maria ni - Mama wa Kanisa na Kanisa ni mwili wa Kristo Mwanaye. Mtaguso unatufundisha kuwa Maria ni mfano ulio kamilifu, ni tunda la kwanza la kanisa. Katika Lk. 8:21 – Yesu anasema wazi kuwa, mama yangu na ndugu zangu ni wale wanaosikia Neno la Mungu na kuliishi.

Liturjia ya leo inaweka mbele yetu Maria kama wa kwanza aliyekuwa mama wa Kanisa kwa jinsi alivyokuwa mwaminifu na msikivu wa Neno lake.

Katika somo hili la kwanza, tunasali sala ya baraka itolewayo kwa watu wa Mungu. Bwana ndilo jina la Mungu, hivyo kuita jina lake ni sawa na kumwita yeye – yaani ukuu wake, upendo wake na amani yake. Kwa Wayahudi - jina linatambulisha au linasimama badala ya mtu mwenyewe, hivyo wanaoliita jina – kwa mfano jina la Mungu – wanamwita Mungu mwenyewe na watapata baraka yake.

Hivyo kadiri ya Andiko hili katika somo hili - wanaoamini na kuungama uwepo wa Mungu humaanisha kuwa wanahitaji baraka yake, wako tayari kupata Baraka yake.
Katika mtazamo huu – Noeli - jina la Yesu ndilo laitwa, yeye ndiye Bwana na mwokozi. Bikira Maria akiwa Myahudi, alikuwa na ufahamu huu - jambo hili lilifanyika wazi hekaluni. Sisi leo tunapooanza mwaka pamoja na Maria, tunaalikwa kuingia katika ufahamu huo.

Katika somo hili twaona wazi wazi matokeo ya ujio na uwepo wa Kristo. Kadiri ya Paulo– aliye mwamini anamhitaji Maria kama vile Mungu alivyomhitaji ili kwake yeye wokovu ufike kwetu. Yesu kwa Neema ya Mungu alizaliwa na mwanamke. Katika Agano la Kale - mwanamke amepata heshima kubwa - Eva Mama wa viumbe vyote. - Mwanzo 3,20. Bkira Malkia - heshima kubwa katika kiti cha ufalme – Lk. 2:19, Isa. 7:14, na Mika. 5:2 - wametaja mama wa masiha – mama ambaye atazaa mtoto, ambaye ni mwokozi.

Injili ni ile ya Noeli –tangazo la Malaika kwa wachungaji na nyimbo za mbinguni kumsifu Mungu. Hapa wachungaji wanafanya kitu- wanaenda kwa haraka kumwona Maria, Yosefu na Mtoto. Wanachoona – ni matokeo ya uwepo wa Kristo - wanamwona Mungu. Bahati gani hii - halafu Maria anayaweka yote moyoni mwake. Anasia mbegu ya Neno la Mungu na kupata sifa na heshima ya kuitwa Mama wa Mungu.

Leo tunaadhimisha sikukuu ya Maria wa Mungu- si kwamba yeye ameanzisha wokovu ila yeye ni yule Bikira mwaminifu aliyemzaa KRISTO Mwana wa Mungu. Ndiyo sababu ya sherehe hii ya leo. Mt. Fransis wa Assisi anasema – sisi tutakuwa Mama zake Kristo kama tukimchukua katika mioyo yetu na katika miili yetu tukiwa na pendo la kimungu na tukiwa safi na salama katika dhamiri zetu. Tutamzaa Yesu katika kazi zetu takatifu ambazo huwa ni mwanga kwa wengine wote. Angalia tena ufahamu wa watu mbalimbali kama manabii kwa mfano – Isa. 7:14 na Mika 5:2.

Kwa njia ya Maria – Mama wa Mungu - alipata upendeleo, akasikia, akatii. Katika moyo wake – ikawepo bustani nzuri ambayo Mungu alisia NENO lake - akapata heshima - Mungu akakaa kwake. Leo tunamheshimu kama Mama wa Mungu. Sisi, wanatuambia watakatifu – tutamzaa Kristo, kama tukimpenda kweli, toka moyoni na katika dhamiri iliyo safi na kama tukitenda yote katika utakatifu na kumwonesha ulimwenguni kwa ushuhuda wa maisha yetu mapya ya kimungu.

Kama mamajusi walivyoenda wakaona, wakaamini, wakamtukuza Mungu - maisha mapya, nasi pia tunaaalikwa leo kufanya upya. Kwa njia ya Maria, ulimwengu ulifanywa upya. Kwa kumzaa mkombozi, ndiye Kristo Bwana. Nasi tunaalikwa pamoja na Maria tuanze upya katika maisha yetu. Tumwombe Mama Maria atuombee kwa Mungu na Mwanae ili tuweze kuanza upya, tunapoanza mwaka mpya siku ya leo.

Mt. Ireneo anasema; UTUKUFU WA MUNGU NI MTU ALIYE HAI na anaongeza kusema; NA UZIMA WA MTU NI KATIKA KUMWONA MUNGU. Maria alimwona Mungu akapata uzima wa milele. Nasi pia iwe hivyo kwetu.
Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.
All the contents on this site are copyrighted ©.