2014-12-30 10:37:38

Vijana ni jeuri ya Kanisa!


Vijana wa Jumuiya ya kiekumene Taizè kutoka katika nchi mbali mbali za Ulaya, ambao kuanzia tarehe 29 Desemba hadi tarehe 2 Januari mwaka 2015 wanakutanika awamu ya thelathini na saba nchini Jamhuri ya Watu wa Czech, inayoadhimisha Jubilee ya Miaka 25 tangu demokrasia ilipojereshwa tena nchini humo, baada ya Wakristo wengi kupoteza maisha yao kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Hili ni kundi la watu lililonyanyaswa na kudhulumiwa, lakini bila kukata tamaa, kiasi kwamba, njia ya uhuru na demokrasia ikapatikana. Vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè wanahamasishwa kushiriki katika hija hii kwa njia ya sadaka ya maisha yao, huku wakijiachilia na kujifunza kutoka kwa Bikira Maria aliyekubali kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili! Injili ya uhai haina budi kukuzwa na kuendelezwa katika undani wa maisha ya vijana.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa vatican kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè kwa mwaka 2015. Baba Mtakatifu anawahamiza vijana kujikita katika mchakato wa sala, majadiliano ya kidini na kiekuemene, ili kweli waweze hatimaye, kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa pamoja na kutambua kwamba, Yesu Kristo ana matumaini makubwa kwa vijana.

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, mapungufu yao ya kibinadamu na umaskini unaowaandama kisiwe ni kikwazo, bali waendelee kumwamini Roho Mtakatifu anaishi na kutenda ndani mwao, changamoto na mwaliko wa kupokea ujumbe wake kwa moyo mkuu, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri pa kuishi kwa kujikita katika umoja na Mwenyezi Mungu pamoja na mshikamano wa kidugu.

Baba Mtakatifu anawaambia vijana kwamba, anawaamini kwa kukirimiwa vipaji mbali mbali pamoja na ugunduzi, ili kweli Injili ya Furaha iweze kuwafikia na kusikilizwa na watu wengi zaidi katika nchi zao. Inapendeza kuwaona vijana wakichakarika kwa ajili ya kushuhudia imani yao na kumtangaza Yesu katika mitaa, barabara na sehemu mbali mbali za dunia.

Vijana ni jeuri ya Kanisa, wanaolihamasisha Kanisa kusonga mbele katika kukamilisha mchakato wa umoja kamili kati ya Wakristo. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuchukua fursa hii kuwatakia kheri na baraka tele katika maadhimisho haya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.All the contents on this site are copyrighted ©.