Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya Kuombea Amani Duniani 2015
Mama Kanisa tarehe Mosi, Januari 2015 anaadhimisha Siku ya Kuombea Amani Duniani inayoongozwa
na kauli mbiu “si tena kama mtumwa, bali ndugu”. Maadhimisho haya yanakwenda sanjari
na Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu.
Baba Mtakatifu
Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Amani Duniani, anaugawa
ujumbe wake katika sehemu kuu mbili, zenye utangulizi unaonesha mpango wa Mungu katika
maisha ya mwanadamu.
Sehemu ya kwanza, Baba Mtakatifu anapembua kwa kina na
mapana mambo mbali mbali kuhusiana na utumwa katika historia ya maisha ya mwanadamu;
sababu zake msingi na sehemu ya pili anaihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kutafuta suluhu
ya pamoja itakayoiwezesha Jamii ya mwanadamu kupambana fika na kashfa ya utumwa ambayo
ni uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Baba Mtakatifu anaanza utangulizi wa ujumbe
wake kwa kumtolea Mwenyezi Mungu sala, ili vita, kinzani na mateso yanayosababishwa
na binadamu yaweze kupata ukomo wake; anasali kwa ajili ya kuombea wale wote ambao
wameguswa kwa namna ya pekee na mlipuko ya magonjwa na majanga asilia na kukumbusha
kwamba, mwanadamu ameumbwa kwa ajili ya kujenga na kudumisha mahusiano na jirani zake
kwa kuzingatia msingi wa haki na mapendo.
Hapa Baba Mtakatifu anawataka watu
kutambua na kuheshimu: utu, uhuru na hali ya mtu kujitegemea, hali ambayo inapaswa
kuonesha mahusiano kati ya watu kwa kukazia kwa namna ya pekee kabisa: heshima, haki
na upendo. Udugu unaopata chimbuko lake kwa kumwongokea Kristo ni kifungo muhimu katika
maisha ya kifamilia na kijamii, hali inayoonesha umoja katika utofauti ulioko kati
ya wanandugu, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wakiwa na asili na utu sawa.
Baba
Mtakatifu anasema, dhambi inapoharibu mshikamano huu wa kidugu, hapo utamaduni wa
utumwa unajipenyeza na kutoa nafasi kwa mtu kumkataa jirani yake, nyanyaso na madhulumu
zinapoonekana; utu na heshima ya binadamu vinatoweka na haki msingi za usawa katika
taasisi zinamong’onyoka. Kutokana na mapungufu yote haya, Jumuiya ya Kikristo haina
budi kuwa ni kielelezo cha umoja kati ya ndugu kwa kuonesha umoja katika utofauti
bila kuathiri utu wala kumtenga mtu yoyote kutoka katika Familia ya Mungu. Hii ni
kwa sababu wote ni watoto wateule wa Mungu wanaoimarishwa kwa kifungo cha udugu katika
Kristo.
Sehemu ya kwanza, katika Ujumbe wa Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka
2015, Baba Mtakatifu Francisko anaangalisha juu ya mabadiliko makubwa ambayo yamejitokeza
katika historia ya mwanadamu kwa kutambua utu na heshima ya binadamu na kwamba, utumwa
ni kitendo kinachodhalilisha na kufisha utu na heshima ya binadamu; jambo ambalo limepelekea
utumwa kupigwa marufu kutoka katika uso wa dunia na kwamba, ni marufuku mtu kuingizwa
katika utumwa, sheria ambao bado inaacha maswali mengi bila ya kuwa na majibu muafaka.
Baba
Mtakatifu anasema hata leo hii, kuna watu wanalazimika kuishi katika mazingira ya
utumwa, kwani kuna mifano hai inayoonesha kwamba, kuna watu wanafanyishwa kazi za
kitumwa; wahamiaji wananyimwa haki zao msingi; wanadhulumiwa na kunyanyaswa; wanawekwa
kizuizini katika mazingira hatarishi; wananyanyaswa na kudhulumiwa na waajiri kwa
kudhibiti mikataba na vibali vya kuishi ugenini.
Kuna wanawake, wasichana
na watoto ambao wametumbukizwa katika biashara haramu ya ngono; wengine wanauzwa kama
biadhaa na kulazimishwa kufunga ndoa za shuruti. Kuna baadhi ya watu wanatumbukizwa
katika biashara haramu ya viungo vya binadamu; watoto wanapelekwa mstari wa mbele
kama chambo katika mapigano ya kivita; kuna baadhi ya watoto wanaolazimishwa kuuza
dawa haramu za kulevya na wengine wanaasiliwa kinyume cha sheria za kimataifa. Kuna
baadhi ya watu wametekwa nyara na kufungwa na vikundi vya kigaidi.
Baba Mtakatifu
anasema, hizi zote ni sura za utumwa mamboleo na kwamba, zina sababu nyingi ambazo
zimepelekea kuendelea kuwepo kwa biashara na utumwa mamboleo. Sababu msingi ni dhambi
inayoathiri moyo wa binadamu kiasi hata cha kuukataa ubinadamu wa mtu mwingine, hali
inayowafanya baadhi ya watu kuwanyanyasa na kuwatumisha binadamu wenzao kama bidhaa
na njia ya kujinufaisha binafsi.
Mambo mengine ni umaskini, ujinga, ukosefu
wa fursa za ajira, biashara haramu ya binadamu na matumizi haramu ya mitandao ya kijamii
inayowafanya vijana wa kizazi kipya kuwa watumwa pamoja na kuvutiwa kujiunga katika
makundi ya kivita, uhalifu, matumizi ya nguvu pamoja na kujihusisha na vitendo vya
kigaidi.
Baba Mtakatifu anasema sababu nyingine zinazopelekea uwepo wa utumwa
mamboleo ni pamoja na rushwa na ufisadi unaojipenyeza katika vyombo vya ulinzi na
usalama kwa kushirikiana na magenge ya uhalifu wa kitaifa na kimataifa, hapa ut una
heshima ya binadamu vinawekwa rehani na badala yake, fedha inapewa kipaumbele cha
kwanza.
Katika sehemu ya pili ya Ujumbe kwa Siku ya Kuombea Amani Duniani,
Baba Mtakatifu Francisko anaihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kushikamana kwa dhati
katika mapambano dhidi ya utumwa mamboleo kwa kujenga na kuimarisha utandawazi wa
udugu. Biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni mambo ambayo yanapata mwanya
kutokana na baadhi ya watu kutojali. Lakini, Baba Mtakatifu anasema, kuna kundi kubwa
la Watawa wa Kike linalofanya utume wake katika hali ya ukimya, ili kuwasaidia waathirika
wa utumwa mamboleo sanjari na kuvunjilia mbali mnyororo wa utumwa unaonyanyasa, dhulumu
na kuwatesa watu kiasi hata cha kuwanyang’anya hati na vitambulisho vyao.
Baba
Mtakatifu anasema kwamba, kwa njia ya ujasiri, uvumilivu na udumifu, Mashirika ya
kitawa yameendelea kuwa karibu zaidi na waathirika wa utumwa mamboleo; kwa kuwasaidia,
kuwapatia ushauri nasaha na hatimaye, kuwaingiza tena katika jamii husika. Jumuiya
ya Kimataifa haina budi kulivalia njuga tatizo hili, ili kuzuia uhalifu, kuwalinda
wahanga pamoja na kuwawajibisha watuhumiwa wa vitendo hivi vinavyodhalilisha utu na
heshima ya binadamu. Hapa kuna haja ya kuwa na umoja na mkakati wa kimataifa kwa kuhakikisha
kwamba, sheria kuhusu wahamiaji, ajira, kuasili pamoja na mgawanyo wa maeneo ya kazi
zinatekelezwa kikamilifu, kwa kulinda, kuheshimu na kutetea utu wa binadamu.
Kuna
haja ya kuwa na sheria zinazosimikwa katika haki na zinazolinda haki msingi za binadamu
bila kutoa mwanya kwa wala rushwa na mafisadi kuendelea “kupeta, huku wakila kuku
kwa mrija” bila ya kuwajibishwa kikamilifu. Wanawake wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa
kutokana na dhamana yao ndani ya Jamii; waajiri wahakikishe kwamba, wafanyakazi wanatekeleza
wajibu wao katika mazingira bora zaidi, kwa kulipwa ujira stahiki, bila ya kujihusisha
na biashara haramu ya binadamu.
Taasisi na Mashirika ya kitaifa na kimataifa
yajifunge kibwebwe kuhakikisha kwamba, yanavunjilia mbali magenge ya uhalifu wa kimataifa,
kwa kuwawajibisha wahusika. Walaji watambue wajibu wao wa kijamii kwani tendo la kununua
linafumbata kanuni maadili na mafao ya kiuchumi.
Baba Mtakatifu Francisko anasema,
Vatican itaendelea kusimama kidete kupinga biashara na utumwa mamboleo kwa kukazia
utandawazi wa kidugu badala ya kuendeza utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko
ya binadamu wengine. Mtakatifu Bhakita awe ni mfano wa matendo ya kidugu kwa wale
wanaoishi katika utumwa. Watu wanapaswa kuhamasishwa kuona nyanyaso na dhuluma wanazofanyiwa
watu wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu zinakoma na kamwe wasibezwe.
Baba
Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa
Mwaka 2015 kwa kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutojihusisha na matendo
yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu; waone na kuguswa na mateso pamoja na
mahangaiko ya binadamu ambao wanapokwa uhuru na utu wao; watu wawe na ujasiri wa kugusa
mateso na mahangaiko ya Kristo kwa njia ya wahanga hawa.
Utumwa mamboleo ni
changamoto ya kimataifa inayoonesha utandawazi usiojali wala kuguswa na mateso ya
watu; uhalifu ambao unapaswa kudhibitiwa kwa kujenga utandawazi wa mshikamano na udugu,
ili kuwapatia wahanga wa vitendo hivi matumaini katika maisha yao!
Na Padre
Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.