2014-12-30 11:33:19

Tarehe 21 Machi 2015 Papa "kutinga timu" Pompei!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 21 Machi 2015 anatarajiwa kufanya hija ya siku moja kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei, yaliyoko kwenye Jimbo kuu la Napoli, Kusini mwa Italia. Taarifa hii imetolewa na Askofu mkuu Tommaso Caputo na kuthibitishwa na Idara ya Habari ya Vatican. Baba Mtakatifu anatarajiwa kwenda huko ili kusali kwa Bikira Maria wa Rozari Takatifu, anayeheshimiwa sana nchini Italia.

Ibada kwa Bikira Maria imekuwa ni chemchemi na kichocheo kikuu cha waamini kuonesha mshikamano a upendo na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko, ni tukio muhimu sana katika mchakato wa kuwaimarisha ndugu zake katika Kristo ili waendelee kujisadaka kwa ajili ya ustawi na mafao ya maskini na wanyonge ndani ya jamii!

Hija hii pamoja na mambo mengine anasema Askofu mkuu Caputo inapania kukazia upendo, haki, utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu anatarajiwa kuwaonesha dira na mwelekeo wa kuendelea kumwilisha imani katika matendo, kwa njia ya huduma.

Itakumbukwa kwamba, kunako tarehe 21 Oktoba 1979, Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea Jimbo kuu la Napoli na kwenye Madhabahu ya Pompei na baadaye alirejea tena kwenye Madhabahu haya kunako tarehe 7 Oktoba 2003, ili kufunga Mwaka wa Rozari Takatifu. tarehe 19 Oktoba 2008, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alitembelea Madhabahu haya.All the contents on this site are copyrighted ©.