Tarehe Mosi Januari, Siku kuu ya Bikira Mama wa Mungu, Theotokos, inayokwenda sanjari
na maadhimisho ya Siku ya 48 ya Kuombea Amani Duniani, inayoongozwa na kauli mbiu
“si tena kama mtumwa bali ndugu”, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza masifu
ya kwanza ya jioni Jumatano tarehe 31 Desemba 2014, majira ya saa 11:00 kwa saa za
Ulaya kwa ajili ya Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu.
Katika masifu
haya, kutakuwa na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha
na utume wa Kanisa na baadaye, waamini wataimba Utenzi wa shukrani, “Te Deum” kama
alama ya kumshukuru Mungu kwa kufunga mwaka wa Serikali. Ibada hii itafungwa rasmi
kwa baraka ya Ekaristi Takatifu.
Alhamisi, tarehe Mosi, Januari 2015, Baba
Mtakatifu Francisko ataunfungua Mwaka kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa heshima
ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Siku ya Kuombea Amani Duniani, kwenye Uwanja wa Kanisa
kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ibada hii inatarajiwa kuanza saa 4:00 asubuhi
kwa saa za Ulaya.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itaendelea kukujuza
yale yatakayojiri katika maadhimisho haya! Tafadhali usikose kumshirikisha jirani
yako!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.