Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury na Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani
anawatakia vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè, heri na baraka kutoka kwa Yesu
Kristo Mkombozi wa dunia, wakati huu wanapokutana mjini Prague, Jamhuri ya Watu wa
Czech, ili kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana wa Taizè
kutoka Barani Ulaya kwa Mwaka 2015.
Anasema, nyakati hizi zinashuhudia tofauti
zinazosababisha hofu, chuki na uhasama kati ya watu; kumbe mkutano huu wa vijana ni
kielelezo cha upatanisho na amani; chachu muhimu sana katika kuharakisha mchakato
wa mageuzi, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amefanyika mwili, ili kuleta mabadiliko
katika ulimwengu, ikiwa kama watu wataweza kuambatana na kushikamana na Yesu katika
maisha yake, ili kweli waweze kupata nguvu ya kujipatanisha wao kwa wao!
Kwa
njia ya Roho Mtakatifu na Fumbo la Pasaka, kila kijana amekirimiwa mabadiliko katika
maisha kwa kupita kutoka katika kifo na kuingia katika maisha mapya; kwa kutoka katika
giza na kuanza kutembea katika mwanga wa maisha ya Kristo. Licha ya mapungufu yanayojionesha
katika maisha ya wanadamu, lakini wanapaswa kukumbuka kwamba, wameumbwa kwa sura na
mfano wa Mungu; wakiwa na utu na heshima inayopata chimbuko lake katika Fumbo la Pasaka.
Vijana
wanakumbushwa kwamba, wao ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu
wa milki ya Mungu, wapate kuziangaza fadhili zake yeye aliyewaita kutoka gizani, ili
waingie katika nuru yake ya ajabu. Kwa watu watakaokubali kielelezo hiki watakuwa
ni watu wapya, watu wa Mungu, wasiojitambulisha kwa utaifa, siasa wala mapambano ya
kutafuta ukuu.
Askofu mkuu Welby anawataka vijana kuendelea kuwa na ndoto ya
kupatanishwa kwa njia ya Roho Mtakatifu, ili kuvuka vikwazo vya kibinadamu; kwa maskini
kupata ukombozi; wafungwa kufunguliwa kwao kutoka katika dhuluma, nyanyaso, dhambi,
chuki; ulaji wa kupindukia, madeni na woga kwa siku za usoni. Kila mtu anapaswa kufahamu
kwamba, amejaliwa uwezo wa kuwa ni raia wa mbinguni, ili kufurahia maajabu ya Mungu.
Vijana wanatakiwa kuendelea kusherehekea kwa furaha huku wakionesha umoja
na mshikamano katika tofauti zao, wakifurahi kufanyika kuwa ni watu wake Kristo kwa
ajili ya huduma!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya
Radio Vatican.