2014-12-30 10:04:30

Ciao 2014! Mwaka uliotanda hofu na wasi wasi mkuu!


Kardinali Francis Arinze anapenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza wafanyakazi wa Idhaa ya Kiingereza na Kiswahili ya Radio Vatican kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa ajili ya kuwahabarisha Watu wa Mataifa kuhusu matukio muhimu yanayoendelea katika maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Vatican. RealAudioMP3

Kardinali Arinze anasema, Mwaka 2014 umesheheni matukio makubwa na muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, hasa wakati huu, Mama Kanisa anapojielekeza zaidi na zaidi katika azma ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mwezi Aprili, Kanisa limewatangaza Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa ni watakatifu, mfano wa kuigwa katika utekelezaji wa Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican; kwa kuendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kimataifa, utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha pekee.

Mwezi Agosti, Baba Mtakatifu Francisko alifanya hija ya kitume nchini Korea ya Kusini, ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo; ili waweze kuwa tayari kutoka kimasomaso kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kanisa nchini Korea ni matunda ya juhudi zilizofanywa na waamini walei, waliokuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya Injili. Leo hii, waamini walei wanahamasishwa na Mama Kanisa kutoka kifua mbele kwenda kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu yanayomwilishwa katika medani mbali mbali za maisha.

Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwaka 2014 ametembelea Nchi Takatifu na Uturuki, kama mhujujaji na chombo cha amani, majadiliano na mshikamano kati ya watu wa mataifa. Ametembelea nchi hizi mbili, ili kuchochea kwa mara nyingine tena ule mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini ulioanzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, yapata miaka hamsini iliyopita.

Lengo ni kuendelea kusimama kidete ili kulinda na kutetea misingi ya haki, amani; majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Ni matumaini ya Kardinali Arinze kwamba, hija hizi za Baba Mtakatifu zitaweza kuzaa matunda kwa wakati wake, jambo la msingi ni kuendelea kuwa na imani na matumaini.

Kardinali Arinze katika ujumbe wake wakati huu wa Noeli anasema kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kujielekeza zaidi na zaidi katika kutafuta, kukuza na kuendeleza misingi ya haki, amani, utulivu na maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Lakini, bado kuna wasi wasi mkubwa umetanda katika uso wa dunia kutokana na dhuluma, nyanyaso na mauaji yanayofanywa kwa misingi ya kidini, kama inavyojitokeza huko: Nigeria, Kenya, Mali, Mexico na Mashariki ya Kati. Kardinali Arinze anawasihi waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kusali kwa ajili ya toba na wongofu wa wale wote wanaofanya vitendo hivi, ili kweli amani, utulivu na maendeleo ya wengi viweze kushika mkondo wake.

Kardinali Arinze anasema, Mwezi Oktoba, kulifanyika Sinodi maalum ya Maaskofu ili kuangalia pamoja na mambo mengine: matatizo, changamoto na fursa zilizopo katika familia, ili Kanisa liendelee kutangaza Injili ya Familia kwa ari na moyo mkuu. Waamini waendelee kuwasindikiza Mababa wa Sinodi katika maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu itakayofanyika mwezi Oktoba 2015 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa familia katika Kanisa na Ulimwengu mamboleo”, ili iweze kuwa na mafanikio makubwa kwa kuwasaidia wanandoa kuishi, kutangaza na kuishuhudia Injili ya Familia.

Kardinali Francis Arinze anasema, kwake Mwaka 2014 ameutumia katika hali ya utulivu kwa kusali, kutafakari pamoja na kutoa mihadhara mbali mbali. Anasema, ikiwa kama itampendeza Mwenyezi Mungu, basi hapo tarehe 29 Agosti 2015, ataadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu na kilele cha tukio hili ni hapo tarehe 28 Novemba 2015 na linatarajiwa kufanyika huko Onitsha, Nigeria.

Kardinali Arinze anawaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kumwombea katika maisha na utume wake. Anawatakia wote kheri na baraka; haki na amani; ustawi na afya njema kwa Noeli na Mwaka mpya wa 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.