Baraza la Maaskofu Katoliki Perù katika ujumbe wake kwa Siku kuu ya Noeli linasema
kwamba, Kipindi cha Noeli ni muda muafaka uliokubalika mbele ya Mwenyezi Mungu, ni
kipindi cha kushirikishana na kumegeana upendo kwa moyo wa ukarimu na majitoleo. Ni
wakati muafaka wa kupandikiza mbegu ya upatanisho, msamaha na amani katika mioyo ya
watu, kwa kushinda chuki, wivu na mashindano yasiyokuwa na tija wala mashiko kwa maisha
na maendeleo ya watu.
Noeli ni
wakati muafaka kabisa wa kujifunga kibwebwe ili kupambana kufa na kupona na ubinafsi
na uchoyo; rushwa na ufisadi mambo ambayo yamekuwa ni sababu ya majanga kwa watu wengi
duniani. Umefika wakati wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi badala ya
kuelemewa na ubinafsi.
Baraza la Maaskofu Katoliki Perù pamoja na mambo mengine
linapenda kutoa kipaumbele cha kwanza kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia;
taasisi ambayo kwa nyakati hizi, inakabiliwa na matatizo na changamoto nyingi ambazo
zinapaswa kufanyiwa kazi, ili Kanisa liweze kutoka kifua mbele kuwatangazia Watu wa
Mataifa Injili ya Familia. Upendo umetoweka ndani ya familia nyingi. Kwa masikitiko
makubwa kuna watoto ambao hawawezi kuzaliwa kutokana na baadhi ya wazazi kukumbatia
utamaduni wa kifo na kutema Injili ya Uhai.
Kuna watoto wanaoishi katika mazingira
magumu kutokana na mafarakano ya wazazi wao na matokeo yake wameachana, hivyo watoto
wanakosa: upendo, malezi na tunza ya wazazi wa pande zote mbili. Hili ni kundi kubwa
la watoto ambalo halina mwelekeo w adira ya maisha. Matokeo kwa watoto kama hawa ni
kutumbukizwa katika biashara haram ya binadamu na utumwa mamboleo, mambo ambayo ni
uhalifu dhidi ya ubinadamu na unyama mkubwa ambao unaendelea kupenya kwa kasi katika
ulimwengu mamboleo. Watoto hawa wote wanaonesha ile sura ya Mtoto Yesu, wanapaswa
kusaidiwa, kulindwa, kupendwa na kutunzwa kwa heshima na upendo mkuu.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Perù linasema kwamba, kuna Wananchi wengi kutoka Perù wanaoishi
ughaibuni, kwa lengo la kutafuta maisha bora zaidi kwa ajili yao na familia zao, wote
hawa wanakumbukwa na Maaskofu katika sala zao, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha
Siku kuu ya Noeli. Wakumbuke kwamba, wanahamasishwa kuchangia kwa hali na mali katika
mchakato wa ujenzi wa nchi yao kwa kujikita katika misingi ya haki, amani, upendo
na mshikamano wa kitaifa; daima wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote
wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Maaskofu wanawatakia wananchi wote amani
na upendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, hakuna mtu yeyote anayetengwa na kazi
ya Ukombozi iliyoletwa na Yesu Kristo, changamoto ya kuchuchumilia Injili ya Uhai
pamoja na kukuza upendo, mshikamano na udugu kati ya watu!
Na Padre Richard
A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.