2014-12-29 09:30:14

Yaliyojiri katika maisha na utume wa Papa Francisko 2014


Mwaka 2014 umekuwa ni mwaka wenye matukio muhimu sana katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko ambaye ameendelea kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana, dhamana ambayo ameitekeleza kwa kufanya hija za kichungaji kimataifa, kwa kukazia majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kuwatangaza Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu, mfano wa kuigwa katika kumwilisha Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika azma ya Uinjilishaji Mpya sanjari na Utangazaji wa Injili ya Familia.

Ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimatifa kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, utu na heshima ya binadamu, kwa kujikita katika uhuru wa kuabudu. Pia ni mwaka ambao Baba Mtakatifu ameutumia katika kuanzisha mchakato wa mabadiliko makubwa katika Sekretarieti ya Vatican kama walivyoagiza Makardinali katika mikutano yao elekezi. Kwa hakika anasema Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican mwaka 2014 umekuwa ni mwaka uliosheheni mchakato wa utamaduni wa watu kukutana!

Padre Federico Lombardi anasema, Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwaka 2014 alitembelea Nchi Takatifu ili kushuhudia: mizizi ya Ukristo, maeneo ya historia ya wokovu kwa kutembelea Mto Yordani, mahali alipobatizwa Yesu kabla ya kuanza maisha ya hadhara. Alitembelea Kaburi Takatifu, linaloonesha Fumbo la Pasaka. Akakutana, akasali na kuzungumza na Patriaki Bartolomeo wa kwanza, kama kilele cha kumbu kumbu ya miaka hamsini ya majadiliano ya kiekumene ndani ya Kanisa, matumaini ya mshikamano wa urafiki na upendo kwa siku za usoni.

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Korea na anayotarajia kuifanya nchini Sri Lanka na Ufilippini ni kuonesha kipaumbele cha pekee kinachotolewa na Mama Kanisa kwa Bara la Asia katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika majadiliano ya kidini na ushuhuda wa imani tendaji. Mama Kanisa anataka kujenga na kudumisha mchakato wa utamadunisho wa Injili kati ya watu na tamaduni za Bara la Asia katika medani mbali mbali za maisha, changamoto ambayo ina magumu yanayopaswa kufanyiwa kazi katika ukweli, uwazi, upendo na mshikamano kwa kukazia mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu ameendelea kuwatia shime Wakristo na watu wenye mapenzi mema Barani Ulaya kwa kutembelea Albania na Strasbourg, Ufaransa; ambako amekazia utu na heshima ya binadamu; demokrasia na mafao wengi, bila kusahau kuwajengea watu matumaini katika maisha. Ushuhuda wa maisha na utume wa Kanisa unaojionesha kwa namna ya pekee katika maisha ya waamini waliojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, wakawa chachu ya maendeleo na ustawi wa Makanisa mahalia, ni mambo msingi ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameyakazia wakati wa hija zake za kitume nchini Albania na Korea ya Kusini na Mashariki ya Kati.

Baba Mtakatifu alipokuwa nchini Albania na Uturuki, amekazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa waamini wa dini mbali mbali kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini, kwa kujiepusha na misimamo mikali ya kidini na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia kwa misingi ya udini. Kuna mambo mengi ambayo waamini wa dini mbali mbali wanaweza kushirikiana ili kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, mafao na maendeleo ya wengi.

Padre Federico Lombardi anasema kwamba, watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II waliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko ni ushuhuda makini wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji, kwa kuendeleza na kumwilisha mageuzi na mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa. Itakumbukwa kwamba, Papa Paulo VI, aliyesimama kidete kulinda na kutetea haki, amani na Injili ya Familia ametangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Mwenyeheri, mwaliko kwa waamini kuendelea kumwilisha Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa vatican katika maisha na utume wa Kanisa.

Maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia ni tukio ambalo liliamsha hisia na changamoto nyingi katika maisha na utume wa Kanisa, tukio ambalo lilifuatiliwa kwa karibu sana na vyombo vya habari, lakini kwa malengo tofauti kabisa. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Familia yamejikita katika hatua mbali mbali kuanzia kwenye mikutano elekezi ya Makardinali, Sinodi maalum na awamu ya tatu ni Sinodi ya Maaskofu itakayofanyika mwezi Oktoba 2015. Familia na Uinjilishaji Mpya ni tema zinazowagusa watu wengi anasema Padre Lombardi, ndiyo maana inatakiwa kujadiliwa kwa umakini mkubwa kwa kuzingatia: ukweli, uwazi, Maandiko Matakatifu, Mapokeo na Mafundisho ya Kanisa.
Familia ni tema muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, ili kuendelea kutangaza Injili ya Familia katika ulimwengu mamboleo unaopambana vikali na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Mama Kanisa anataka kuimarisha: imani, matumaini na mapendo katika maisha ya ndoa na familia, kwa kujikita zaidi na zaidi katika maisha ya Kikristo. Matatizo na changamoto ni sehemu ya maisha ya binadamu, zinapaswa kukabiliwa kwa ujasiri na moyo mkuu.

Padre Lombardi anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kwa Mwaka 2014 amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha haki, amani, utu na heshima ya binadamu, kwa kuendelea kushikamana kwa hali na mali na watu wote wanaodhulumiwa na kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kama inavyotokea sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa namna ya pekee huko Mashariki ya kati. Kuna maelfu ya watu wameuwawa na wengine kulazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na chuki za kidini.

Bado kuna wimbi kubwa la biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, mambo ambayo ni uhalifu mkubwa dhidi ya ubinadamu. Mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni changamoto inayohitaji ushirikiano wa dhati na Jumuiya ya Kimataifa pamoja na watu wenye mapenzi mema, ndiyo maana Baba Mtakatifu ameungana na viongozi mbalimbali wa kidini ili kuhakikisha kwamba, kwa pamoja wanasimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu dhidi ya nyanyaso.

Baba Mtakatifu Francisko anaendeleza mabadiliko katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kukazia dhana ya Umissionari wa Kanisa linalotoka kifua mbele ili kuwatangazia watu Injili ya Furaha; Kanisa linalojielekeza katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anaendelea kufanya marekebisho katika Sekretarieti ya Vatican, jambo linalohitaji subira, ukweli, uwazi na ujasiri.

Marekebisho makubwa yanapaswa kufanywa na wahusika kutoka katika undani wa maisha yao, kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani; kwa kuganga na kutibu madonda ya ndani, ili kujikitz katika tunu msingi za Kiinjili na huduma kwa Kristo na Kanisa lake. Viongozi wa Kanisa wajenge utamaduni wa kusikiliza, kujadiliana, kusaidiana na kuhudumiana; wawe tayari kujisafisha na kujitakasa mbele ya Kristo na changamoto za mwanga wa Injili.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga utamaduni wa watu kukutana, kuthaminiana na kupendana kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, tofauti zao zisiwe ni sababu ya chuki na kinzani, bali mahali muafaka pa kukutana na kusaidiana zaidi kwa kukuza utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; katika maisha na utume wa Kanisa unaojikita katika majadiliano ya kiekumene na kidini; kisiasa na kidiplomasia kama ilivyotokea kwa Cuba na Marekani kuanzisha tena mchakato wa mahusiano ya kidiplomasia.

Ni utamaduni unaopania kukuza na kudumisha utu, heshima na mafao ya binadamu wote. Utamaduni wa kukutana na watu upate chimbuko lake katika undani wa maisha ya watu; kiroho, kidini, kiekumene, kisiasa na kiuchumi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.