2014-12-29 09:29:39

Wekezeni kwenye familia kwani inalipa sana!


Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza wanachama wa Chama cha Umoja wa Wanafamilia wengi nchini Italia, waliofika mjini Vatican kutoka mjini Brescia, alikozaliwa Mwenyeheri Papa Paulo VI, ili kusherehekea pamoja Siku kuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, Jumapili tarehe 28 Desemba 2014. Wao ni kielelezo kwamba, familia hizi zinapenda kulinda na kutangaza Injili ya Uhai.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amewaambia kwamba, Familia ni kielelezo tosha cha watu kutaka kukutana na kusaidiana kwa hali na mali. Familia hizi zimefika mjini Vatican zikiwa zimesheheni zawadi ya ubaba na umama inayopokea na kukumbatia uhai. Ikumbukwe kwamba, watoto ni zawadi maalum katika historia ya maisha; ni kundi linaloleta mabadiliko ya mfumo na mtindo wa maisha ya familia. Watoto ni maajabu ya Mungu yanayochochea mabadiliko ya kina; ni matunda ya upendo kati ya Baba na Mama, wanaokuwa na kukomaa katika upendo.

Watoto wanaotoka kwenye familia za watu wengi, wana uwezo wa kujenga udugu na mshikamano tangu wakiwa watoto wadogo tofauti kabisa na ubinafsi unaoendelea kuwameza watu wengi kwa nyakati hizi. Familia zenye watoto wengi ni shule ya mshikamano na umoja, tunu msingi katika maisha ya kijamii. Watoto ni matunda ya familia yenye mizizi yake kutoka kwa wazee. Familia ya binadamu ni sawa na msitu mkubwa unaozaa matunda ya mshikamano, umoja, imani, msaada, usalama, kiasi, furaha na urafiki. Ni kielelezo cha matumaini ya jamii, kwa kusaidiana na kurithishana imani, maadili na utu wema.

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, wazee wengi Barani Ulaya wamekuwa ni chachu ya imani kwa wajukuu wao, kwani wamewasaidia kupata imani kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo pamoja na kuendelea kuwarithisha imani, matumaini na mapendo katika hija ya maisha yao.

Baba Mtakatifu anawapongeza wazazi kwa kupenda na kuthamini zawadi ya Uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Hii ni dhamana nyeti inayotekelezwa katika mazingira magumu na wakati mwingine pasi na msaada kutoka Serikalini, hata kama kuna sera na mikakati ya kusaidia familia zenye watu wengi, lakini sera hizi zimebaki katika maneno tu.

Baba Mtakatifu Francisko anachukua fursa hii kuwahamasisha wanasiasa na watunga sera nchini Italia kuhakikisha kwamba, wanaunga mkono juhudi za familia hizi, kwani kila familia ni chanzo cha jamii husika, lakini familia zenye watoto wengi zina utajiri mkubwa kwa jamii, kumbe, Serikali inapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa kuwekeza kwenye familia kama hizi, ili ziweze kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara.

Baba Mtakatifu anavihamasisha vyama na mashirika ya kitume yanayojikita katika familia, kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika medani za kisiasa na kijamii ili waweze kuchangia katika utungaji wa sera na mikakati kwa ajili ya familia, kwa kutetea na kulinda tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Vyama hivi vya kitume vijitokeze hata katika maisha na utume wa Kanisa mahalia.

Baba Mtakatifu anasema, ataendelea kuwasindikiza katika sala na maombi yake na anapenda kuwaweka chini ya ulinzi, usimamizi na tunza ya Familia Takatifu ya Nazareti. Anawashukuru na kuwapongeza kwa kujenga nyumba mjini Nazareti kwa ajili ya familia kutoka sehemu mbali mbali za dunia zinazokwenda kufanya hija katika Nchi Takatifu.

Baba Mtakatifu anaendelea kuziombea familia ambazo zimeathirika kutokana na myumbo wa uchumi kimataifa, kwa kukosa fursa za ajira; familia zinazokabiliana na na matatizo pamoja na changamoto mbali mbali za maisha, kamwe zisikate tamaa na hatimaye, kutumbukia katika upweke hasi, kinzani na migawanyiko. Kila mtu aweze ni kielelezo cha upole na faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.