2014-12-29 15:16:02

Utoto Mtakatifu Jimbo kuu la Dar es Salaam!


Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jumatatu tarehe 29 Desemba 2014 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu ya Watoto Mashahidi waliouwawa kikatili na Mfalme Herode, aliposikia kwamba, kuna Mfalme amezaliwa mjini Bethlehemu.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku kuu ya Noeli aliwakumbuka kwa namna ya pekee, watoto wanaoendelea kufutiliwa mbali na upanga wa Herode kutokana na magonjwa, ukatili, nyanyaso na vita na hata wakati mwingine mbele ya macho ya waamini na Jumuiya ya Kimatifa.

Shirika la Kimissionari la Kipapa la Utoto Mtakatifu, Jimbo kuu la Dar es Salaam, kila mwaka linaadhimisha kumbu kumbu ya Watoto Mashahidi kama siku yao maalum, inayowakusanya watoto kutoka katika Parokia zote za Jimbo kuu la Dar es Salaam, ili kumzunguka Kardinali Polycarp Pengo, aweze kuwatia shime na ari ya kuwa ni Wamissionari kati ya watoto wenzao.

Kardinali Pengo katika mahubiri yake, amewataka watoto kuiga mfano bora wa Mtoto Yesu katika maisha na makuzi yao, kwa kutambua, nafasi, dhamana na utume wao ndani ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake. Watoto wakiandaliwa barabara wanaweza kutekeleza mambo makubwa katika maisha na utume wa familia na wala si watu wa kutumwa peke yake.

Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu walipompeleka Mtoto Yesu, Hekaluni, alibaki nyuma, akiwafundisha wakuu wa makuhani kama sehemu ya utekelezaji wa mapenzi ya Baba yake wa Mbinguni. Hata wazazi wake waliporudi Hekaluni na kumkuta akiwa amezungukwa na wakuu wa Makuhani, wazazi wake hawakuwa na wasi wasi, bali walishangaa, Je, mtoto huyu atakuwa ni wa namna gani? Yesu alikuwa anafundisha na kujibu maswali kwa ufundi mkubwa, kiasi cha kuwaacha wataalam na mabingwa wa Maandiko Matakatifu wakiwa wameshikwa na bumbuwazi.

Kardinali Pengo amewataka watoto kuwa macho na makini katika mazingira na makundi yanayowazunguka, kwani yanaweza kuwatumbukiza katika mambo ambayo yanaweza kumong’onyoa maadili na utu wema, kwa kuwapotosha katika maisha yao! Watoto wamweke Kristo mbele ya macho yao, wanapokabiliana na changamoto za maisha; daima wajitahidi kumshirikisha katika maamuzi na maisha yao ya kila siku. Kwa kufikiri na kutenda kadiri ya Yesu, watoto hawa wanaweza kuwashangaza wengi, kwani watatambulikana kutokana na tofauti yao na watoto wengine.

Kardinali Pengo amewataka watoto kuachana na tabia mbaya zinazowafanya baadhi yao kuwa ni wadokozi, kukosa maadili na kuwa na lugha chafu za matusi. Watoto watambulikane kwa kumuiga na kuishi kama Mtoto Yesu, ili waweze kuwapiga bumbuwazi, wale wanawazunguka katika maisha. Watoto waongozwe katika maisha yao na hekima pamoja na mapenzi ya Mungu.

Kardinali Pengo amehitimisha mahubiri yake, kwa kuwatakia watoto wote tunza ya Mtoto Yesu, ili aweze kukaa pamoja nao, kwa kuwaongoza na kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani.

Na Padre Agapito Mhando,
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.