Tangazeni Injili ya Familia kwa njia ya ushuhuda wa maisha!
Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, iliyoadhimishwa
na Mama Kanisa jumapili tarehe 28 Desemba 2014, ni sehemu ya maandalizi ya kina kwa
ajili ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, itakayofanyika mjini Vatican
kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015.
Katika mahojiano
maalum na Radio Vatican, Askofu Joseph Mlola wa Jimbo Katoliki Kigoma, Tanzania, anawataka
waamini kutambua kwamba, wao kimsingi wanaunda Familia ya Mungu, Kanisa dogo la nyumbani,
changamoto na mwaliko kwa kila mwamini kujisikia kuwa ni sababu ya umoja, mshikamano
na mapendo ndani ya familia, sanjari na kuendelea kuiga mfano bora kutoka kwa Familia
Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.
Askofu Mlola anawataka wanafamilia kujenga
na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa kujikita katika tabia njema
ya: kusamehe na kusahau; ya kutoa na kupokea msamaha; ya kumwomba na kumshukuru Mungu
pamoja na jirani, kwani falsafa ya neon asante ni kuomba tena!
Askofu Mlola
anazitaka familia kuwa na ujasiri, moyo na utamaduni wa kusahihishana na kurekebishana
kwa imani, mapendo na udugu, ili familia ziweze kuwa wamoja kama ilivyokuwa kwa Familia
Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.