2014-12-29 08:57:09

Mapadre!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo. Mtaguso Mkuu wa II wa Vaticani unaendelea kukunong’onezea mambo mema, ili uweze kuwa Mwamini hai, mwenye kujua na kutimiza wajibu wako vema ndani ya Kanisa. RealAudioMP3 00:11:58:46

Leo tunalitazama agizo la Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican linaloitwa kwa lugha ya Kilatini ‘Presybiterorum Ordinis’, ikimaanisha ‘daraja ya mapadre’. Ndanimwe imesheheni utume na maisha ya mapadre, na pia wajibu wetu sisi kama waamini kwa mapadre. Kuna wajibu wa kiroho na wajibu wa kijamii. Leo tutapigia mistari sana wajibu wetu wa kijamii kwa mapadre wetu.

Kukukumbusha tu mpendwa msikilizaji katika Kanisa letu hili zuri sana, kuna daraja tatu za wahudumu wa Daraja Takatifu. Daraja la kwanza ni Maaskofu, hao huwekwa wakfu na Mama Kanisa, ili kulichunga kundi la Mungu. Maaskofu, wana utimilifu wote wa Upadre. Ni kwa sababu hiyo, maaskofu peke yao ndio huweza kutoa sakramenti ya daraja takatifu kwa wengine. Daraja la pili, ndilo la Mapadre. Hao hushirikiana na Maaskofu katika masuala ya kichungaji.

Upadre ni daraja takatifu ngazi ya pili. Na daraja la tatu ni Ushemasi. Hao humsaidia Askofu na Padre katika huduma kwa kundi la Mungu. Kipindi kilichopita tulidadafua kidogo juu ya huduma ya Maaskofu katika Kanisa. Leo tunawatazama Mapadre katika Kanisa kwa mwangwi wa hati hii tuliyokwishakuitaja.

Sura ya kwanza inatueleza juu ya Upadre kama Utume ndani ya Kanisa. Utume huo unawaunganisha Maaskofu na Mapadre kwa ajili ya kulihudumia taifa la Mungu. Askofu naye kimsingi ni Padre, lakini ni Padre mwenye utimilifu wa upadre. Padre hupewa daraja hili na Askofu. Na yeyote mwenye kupokea daraja la Upadre hapokei kwa ajili yake, bali kwa ajili ya utume. Padre anapewa mamlaka na nguvu kwa ajili ya utume ndani ya Kanisa. Utume kwa kunena siri za Kristo, kuadhimisha mafumbo ya Mungu kwa ajili ya wokovu wa roho za watu.

Sura ya pili inafafanua zile kazi tatu za mapadre, ambazo wanazishiriki kutoka kwa Askodu yaani kufundisha, kutakasa na kuongoza. Na kwa namna ya pekee sura hii inaelekeza juu ya uhusiano wa Mapadre na Askofu wao uweje na pia uhusiano kati yao, na tena uhusiano wao na waamini walei uweje.

Na katika sura inayofuata, tunaona jinsi ambavyo sisi walei tunawajibika kwa Mapadre wetu. Kama wao wanawajibika kwa maisha yao yote kwa ajili ya wokovu wa roho zetu, sisi nasi tunawajibika kwa namna fulani kwa ajili ya usitawi na hali njema yao. Ndipo hati hii inatualika sisi waamini kuwasaidia mapadre wetu kwa namna mbalimbali; iwe kwa maisha ya kiroho, kuhusu elimu yao na kuhusu malipo ya haki na bima, hati inasema ‘ili wasije wakahangaika’. Mwishoni mapadre wanatiwa moyo katika magumu yanayowakabili siku hizi, kwa kukumbusha kinachojulikana kwa tu, kwamba na Kanisa wapo pamoja nao.

Mpendwa msikilizaji, mara nyingi tumehimizwa juu ya kuwalea vizuri watoto wetu katika misingi ya imani na maadili mema, ili mbegu njema ya wito wa huduma ya altare iweze kuwaka mioyoni mwa watoto wetu, ikue na ichipue ili siku mmoja wajekuwa ni waadhimishaji na wagawaji wa mafumbo ya Mungu katika Altare Takatifu ya Mungu. Na kuna baadhi ya sehemu ambako kwa kweli kuna ukame wa miito. Hatupati mapadre kabisa. Waliopo ni wachache, hawatoshi na pengine wamechoka vibaya.

Kwa njia ya tafakari ya hati hii, tukumbuke kwamba, ‘mapadre wanatoka kwetu wenyewe na kwa ajili yetu’. Ni wajibu wa kila moja ndani ya Kanisa Takatifu, kuombea usitawi na udumifu wa miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Na kule kwenye familia zetu, kwenye ndoa zetu, tusikwepe wala kuogopa wajibu wa kuzaa watoto na kuwatunza vyema. Utamaduni wa siku zetu hizi, unaangamiza miito kabisa. Wengi wanapenda kuwa na mtoto mmoja tu, au wawili. Sasa katika familia tukizaa mtoto mmoja, nani atakuwa Padre na nani atakuwa Daktari na nani atakuwa Askari? Tulitazame hilo neno, kwa jicho wajibifu!

Lakini pia, tukumbuke, Mapadre wana wajibu wa kutulisha sisi kwa neno na kwa sakramenti kwa njia ya maadhimisho ya altare na kwa njia ya ushauri wao mwema kwetu. Kila Padre aliyewekwa wakfu, ni kuhani mkuu anayempendeza Bwana katika maadhimisho Matakatifu. Ndiyo maana katika mafundisho yetu maalumu ya ndani sana, tunaelekezwa kwamba, hata kama Padre anaonekana hapendezi katika macho yetu kwa sababu iwayo yoyote, lakini Padre huyo akiadhimisha mafumbo matakatifu kwa ajili ya taifa ya Mungu, taifa la Mungu linabarikiwa kweli.

Padre huyo akiwabariki, mnabarikiwa kweli. Kwa nini?? Kwa sababu padre yoyote hufanya kazi katika Nafsi ya Kristo na kwa jina la Kanisa! Mungu mwema na mwenye huruma, hutumia hata viumbe wanyonge na wadhaifu sana kwa ajili ya wokovu wa watu wake.
Kwa mantiki hiyo sisi waamini, tujitahidi na tujitume sana kuwatunza na kuwasaidia mapadre wetu. Msaada wa kwanza kabisa ni sala. Tuwaombee kila mara. Shetani anajua vizuri sana nguvu na mamlaka ya Padre kuliko mwamini anavyojua. Ndiyo maana mapadre daima huelekezewa mashambulizi mbalimbali na shetani. Shetani anataka kumpiga sana mchungaji ili kondoo watawanyike. Ndio hapo tunapoomba na kusihi sana utume wa sala kwa ajili ya mapadre wetu.

Wakati mwingine sisi waamini tunashika utume wa kuwasemasema, kuwakorofisha, kuwakwaza na hata kuwabinafsisha na kuwaangusha mapadre wetu badala ya kuwaongoza. Hapo tunamsaidia shetani ili kufanikisha miradi yake. Tuwaombee, na tuwape nafasi ili watuchunge vema.

Pamoja na wajibu wetu wa kuwaombea, kadiri ya hati hii sisi waamini tunao wajibu wa kijamii kwa mapadre wetu, yaani kuwasaidia katika mahitaji yao ya maisha. Kuwakimu katika maisha yao. Huwa inakuwa aibu sana mapadre wetu wanapoonekana kuchoka na kuchakaa na kuhangaika kwa maisha duni na ya tabu, yenye damu tupu na vidonda, wakati waamini tupo, tunasitawi vizuri katika majumba ya kifahari, tunakula na kunywa huku mapadre wetu wapiga miayo ya kukata tamaa.

Hapa mwito unatolewa kwa waamini wote kujiuliza: tunawatunzaje mapadre wetu? Familia zetu zinachangia nini kwa maisha ya mapadre wetu? Katika umoja wetu sisi kama Parokia, hatushindwi kuwatunza mapadre wetu. Kuwajengea nyumba nzuri ya kisasa ya kuishi, kuhakikisha wanakula vizuri, wanavaa vizuri hadi Altareni, wanalala mahali pazuri na zaidi kuwahakikishia matunzo mazuri ya afya kwa kuwaandalia bima za afya, na mwisho kujitahidi kuwawekea akiba ya uzeeni.

Yaani mapadre wetu katika uzee wanatia huruma mno kwa jinsi tunavyowatelekeza katika umasikini na upweke mkuu. Kuna aina fulani ya kumwachia Askofu wajibu wote wa kuwatunza mapadre waliopo kazini na wazee. Na hiyo hali duni ya mapadre wawapo kazini na uzeeni ni moja ya sababu-mlenda zinazochangia kuzorotesha miito.

Sote tuamke kabisa, tujitathimini na tuchukue wajibu wa kuwasaidia Mapadre wetu kwa mfumo sahihi unaojumuisha waamini wote katika Parokia. Namna mojawapo ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya mapadre katika Kanisa ni kuwatunza. Sisi waamini tunaamini kwamba tunaweza kabisa ila hatujaamua kuanza kutekeleza kikamilifu wajibu huu.

Endapo Padre wa parokia yetu ataonekana amekondakonda kwa njaa, ni aibu yetu sisi waamini wake, tena aibu kubwa sana! Tukivitunza vyema vyombo hivi vya Mungu, Mungu naye atatubariki zaidi. Tusisahau kuwapelekea mapadre wetu zawadi ya Heri ya Noeli na Mwaka Mpya; kabla ya kupeleka zawadi hakikisha umefuata sheria, kanuni na taratibu za kodi, vinginevyo unaweza kusababisha majanga!
Nami nikikutakia heri tele na baraka tele kwa sherehe za Noeli na Mwaka Mpya 2015
Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martini Mkorwe, OSB.
All the contents on this site are copyrighted ©.