2014-12-29 10:44:17

Injili ya Familia na changamoto zake!


Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na walles, kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia itakayoadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2014, kwa kuongozwa na kauli mbiu "Wito na utume wa Familia katika Kanisa na Ulimwengu mamboleo", limechapisha vitini vinavyopania kuwapatia waamini nafasi ya kutafakari kuhusu wito, safari na utume wa familia nchini humo.

Waamini wanahamasishwa kujitaabisha kuyafahamu mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu maisha ya ndoa na familia, kama sehemu ya mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, inayoingia sasa awamu ya pili!

Vitini hivi ni sehemu ya changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko mwezi Oktoba 2014, alipowataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kufanya tafakari ya kina kuhusu maisha ya kiroho, mintarafu matatizo, changamoto na fursa zilizoibuliwa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia iliyohitimishwa hivi karibuni mjini Vatican.

Waamini waangalie changamoto hizi na kujitahidi kuzipatia majibu muafaka katika maisha na utume wa Kanisa, huku wakiendelea kumwomba Roho Mtakatifu, ili aliwezeshe Kanisa kuendeleza mchakato huu wa tafakari ya maisha ya kiroho, kuhusu utume na maisha ya ndoa ndani ya Kanisa. Waamini waoneshe njia ambazo Mama Kanisa anaweza kuzitumia katika kuimarisha maisha na utume wa Kanisa, ili waamini waendelee kutangaza Injili ya Familia kwa watu wa nyakati hizi, kwa ari na moyo mkuu zaidi!

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza, linawawekea waamini mifano bora ya kuigwa kutoka katika Maandiko Matakatifu, hawa ni Abraham na Sara, kutoka katika Agano la Kale; Simulizi la Bikira Maria kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu kama lilivyoandikwa na Mwinjili Luka, Arusi ya Kana na Yesu alipokutana na Wanafunzi wa Emmau.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza linafafanua kwa kina na mapana kuhusu Sakramenti ya Ndoa pamoja na Mafundisho ya Kanisa kuhusiana na utume na maisha ya ndoa na familia za Kikristo, changamoto na mwaliko kwa waamini kujikita katika uaminifu, udumifu, upendo, daima wakiwa tayari kupokea na kukumbatia Injili ya Uhai, ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Waamini wanaswalishwa kuangalia, Je, ni mambo yepi yanayosababisha furaha na matumaini kwa familia za Kikristo leo hii? Je, ni upi utume wa familia? Ni namna gani wanafamilia wanaweza kutajirishana kimaadili, kiutu na kijamii kwa kuzingatia Mafundisho ya Kanisa? Je, ni kwa giasi gani, familia zimekuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa kwa maneno na matendo yao?. Mwishoni, Maaskofu wanawapatia waamini Sala ya Familia iliyotungwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 27 Oktoba 2013 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Familia.All the contents on this site are copyrighted ©.