2014-12-29 09:28:46

Familia Takatifu ni cheche ya matumaini kwa binadamu!


Katika furaha na shamrashamra za Siku kuu ya Noeli, Mama Kanisa Jumapili tarehe 28 Desemba 2014 ameadhimisha Siku kuu ya Familia Takatifu ya Nazareti. Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu, baada ya siku arobaini, wanampeleka Mtoto Yesu Hekaluni kadiri ya sheria ya Musa, ili aweze kutolewa kwa Mwenyezi Mungu. Katika umati mkubwa wa watu uliokuwa umefurika Hekaluni pale ni Mzee Simeone na Anna waliokuwa wameongozwa na Roho Mtakatifu waliobahatika kumtambua na kumshukuru Mungu kwa uwepo wa Masiha kati yao.

Yesu anayakutanisha makundi makuu mawili, kundi la vijana linaloundwa na Maria na Yosefu pamoja na kundi la pili la wazee linaloundwa na Mzee Simeone na Anna; watu waliosheheni imani na furaha. Yesu anakuwa ni daraja linalounganisha vizazi, chemchemi ya upendo inayounganisha familia na watu mbali mbali, ili kushinda hali ya kudhaniana vibaya, utengano pamoja na kufupisha umbali kati ya watu. Wazee wanayo nafasi ya pekee katika maisha na utume wa familia na jamii katika ujumla wake na kwamba, mahusiano mema kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya ni muhimu sana katika hija ya Jumuiya za Kikanisa na Kijamii.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana, Siku kuu ya Familia Takatifu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, uliokuwa umefurika kwa umati mkubwa wa familia kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu anasema, Familia Takatifu ni wajumbe wa imani wanaotoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mungu kati yao na kwa namna ya pekee kabisa, Yesu Kristo, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Uwepo wa Yesu ni kiini cha utakatifu wa Familia Takatifu. Hii ina maana kwamba, familia zinapojikita katika imani zinapata nguvu ya kuweza kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto mbali mbali kama ilivyotokea kwa Familia Takatifu ya Nazareti, ikalazimika kukimbilia Misri, ili kuokoa maisha ya Mtoto Yesu.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Familia Takatifu ni mwanga angavu unaopenyeza huruma na ukombozi wa Mungu kwa wanadamu. Ni mwanga unaosheheni ukweli kwa kila mwanadamu. Ni mwanga unaoleta faraja kwa familia ambazo kwa sababu mbali mbali zinakosa amani, upendo na msamaha. Huu ni mwaliko kwa waamini kuonesha mshikamano wa dhati na familia ambazo zinakabiliana na hali ngumu ya maisha kutokana na magonjwa, ukosefu wa fursa za ajira, ubaguzi, utengano na hali ya kutoelewana kati yao pamoja na kulazimika kukimbilia ugenini. Hapa Baba Mtakatifu amewaalika waamini kusimama kwa kitambo kidogo, ili kusali kwa ajili ya kuziombea familia zote hizi.

Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria azisaidie familia ili ziweze hatimaye, kuishi katika imani, umoja kwa kusaidiana pamoja na kuendelea kupata tunza ya kimama kutoka kwa Bikira Maria.

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko aliyaelekeza mawazo yake huko Malaysia, ambako kuna ndege ya abiria iliyopotea angani wakati ikifanya safari kutoka Indonesia kwenda Singapore. Amewakumbuka watu kadhaa waliopata ajali huko kwenye Bahari ya Adriatic; wote hawa anapenda kuwaonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na faraja kwa familia, ndugu na jamaa wote waliofikwa na majonzi katika mazingira yote haya. Anawatia shime wale wote wanaojibidisha katika zoezi la kuokoa maisha ya watu waliopata ajali hizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.