2014-12-29 10:04:32

Askofu mkuu Pittau, Mmsionari wa Japan amefariki dunia!


Baba Mtakatifu Francisko, amepokea kwa masikitiko makubwa habari za kifo cha Askofu mkuu Giuseppe Pittau, aliyewahi kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la elimu Katoliki kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2003. Askofu mkuu Pittau amefariki dunia tarehe 26 Desemba 2014, huko Tokyo, Japan, akiwa na umri wa miaka 86.

Baba Mtakatifu Francisko, katika salam za rambi rambi alizomtumia Padre Adolfo Nicolas Pachon, Mkuu wa Shirika la Wayesuit, anamkumbuka Marehemu Askofu mkuu Pittau kutokana na bidii na juhudi zake katika utume wake kwa Mungu na utangazaji wa Injili. Amekuwa ni kiongozi aliyejisadaka kwa ajili ya umissionari kama Gombera wa Chuo kikuu cha Sophia, Tokyo na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregoriani, kilichoko mjini Roma.

Wakati huo huo, Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anamkumbuka Marehemu Askofu mkuu Pittau kuwa ni mmissionari mahiri, akiwa na umri wa miaka ishirini na minne, alitumwa na Shirika la Wayesuit kwenda kutangaza Habari Njema nchini Japan, huko akafundisha na kuongoza, akasimamia mchakato wa elimu hata nyakati za mageuzi ya elimu nchini Japan.

Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alipofanya hija ya kichungaji nchini Japan, Padre Pittau alikuwa ni kiongozi wake, kiasi cha kujenga urafiki na imani na Padre Pittau. Aliwahi kuwa ni kati ya washauri wakuu wa Mkuu wa Shirika la Wayesuit, duniani. Askofu mkuu Pittau baada ya kutimiza miaka 75, alirejea tena mjini Tokyo, Japan, akiendelea na huduma zake za kichungaji kama Kuhani wa kawaida tu. hadi pale mwenyezi Mungu alipomwita mbele ya haki, huku akiwa na matumaini katika ufufuko na maisha ya uzima wa milele.All the contents on this site are copyrighted ©.