Agca aweka shada la maua kwenye Kaburi la Yohane Paulo II, miaka 30 baada ya kukutana
gerezani!
Mehemet Ali agca, kutoka Uturuki aliyempiga risasi Baba Mtakatifu Yohane Paulo II
kunako mwaka 1981, Jumamosi tarehe 27 Desemba 2014 alikwenda kwenye Kanisa kuu la
Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kutoa heshima zake kwa Mtakatifu Yohane Paulo II
na akafanikiwa kuweka shada la maua. Ali Agca alisamehewa na Baba Mtakatifu Yohane
Paulo II alipomtembelea gerezani na baadaye Rais Carlo Azeglio Ciampi akamsamehe na
hatimaye, kuruhusiwa kutoka nchini Italia kunako mwaka 2000.
Tukio la Ali Agca
kutembelea na kuweka shada la maua kwenye Kaburi la Mtakatifu Yohane Paulo II limekwenda
sanjari na kumbu kumbu ya miaka thelathini na moja, tangu Baba Mtakatifu Yohane Paulo
II alipomtembelea Agca kwenye gereza la Rebbibia, kunako Desemba 1983. Ali Agca aliingia
Kanisani kwa uhuru kamili kwani hakuna kizuizi chochote kutoka Vatican anasema Padre
Ciro Benedettin, Msemaji msaidizi wa Vatican.
Ali Agca baadaye alikamatwa na
Askari wa Italia ili kuhojiwa ikiwa kama alikuwa na nyaraka zilizomwezesha kuingia
nchini Italia, lakini kwa bahati mbaya hakuwa wala kibali cha kuingia nchini Italia,
hivyo Jeshi la Polisi nchini Italia, limemfukuza nchini humu. Ali Agca kwa mara mbili
mfululizo ameomba kukutana ili kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, lakini hajawahi
kupata kibali, Padre Lombardi anasema, shada la maua kwenye Kaburi la Mtakatifu Yohane
Paulo II linatosha!