2014-12-27 11:24:40

Wananchi wamechoshwa na vita!


Askofu mkuu Dieudonnè Nzapalainga wa Jimbo kuu la Bangui ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu katoliki Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati anasema, wananchi wamechoka na vita, kinzani na misigano ya kijamii, wanataka kuona tena: haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa vinatawala sanjari na kudumisha utawala wa sheria, ili kulinda usalama wa raia na mali zao.

Wasi wasi bado umetanda kiasi cha kudhohofisha mchakato wa utoaji wa huduma na uzalishaji mali. Watu wanapaswa kubadilika na kuachana na maovu tayari kuanza ukurasa mpya wa maisha, kwa kujikita katika misingi ya haki, amani, msamaha na upatanisho wa kweli. Badala ya kuendelea kuendekeza kinzani na migogoro ya kidini, watu wajiimarishe katika kukuza umoja, udugu na mshikamano, kwa kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao.

Vijana ni kundi ambalo linatumiwa na wanasiasa waliofilisika kwa mafao yao binafsi, changamoto kwa Kanisa kuanzisha mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji utakaoliwezesha Kanisa kuwasikiliza vijana kwa makini na kuwasaidia kwa hali na mali katika majiundo yao awali na endelevu, kwa kuwajengea dhamiri nyofu inayowawajibisha mbele ya Mungu na Jamii inayowazunguka.

Vijana wengi wanatafuta furaha ya kweli katika maisha, wakisaidiwa kwa njia ya tunu msingi za Kiinjili, wanaweza kuwa watu wema na watakatifu. Vijana wafundwe kuwa ni vyombo vya haki, amani na upatanisho; mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha kwanza na Mama Kanisa wakati huu wa Kipindi cha Noeli.

Askofu mkuu Nzapalainga anasema, Jumuiya ya Kimataifa bado ina dhamana kubwa ya kuwasaidia wananchi wa Afrika ya Kati ili kukabiliana na changamoto zilizopo kwa sasa, ili nchi yao isigeuzwe kuwa ni pango la wevi, mafisadi na wanyang'anyi. Lakini wananchi wanakumbushwa kwamba, amani kimsingi ni wajibu wa wananchi wa Afrika ya Kati na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inachangia pale ambapo wananchi wenyewe wameonesha nia ya kuanza ukurasa mpya, vinginevyo ni sawa na kumpigia mbuzi, gitaa!

All the contents on this site are copyrighted ©.