2014-12-27 10:56:41

Kampeni za uchaguzi mdogo Zambia zimepamba moto!


Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia katika maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 tangu Zambia ilipojipatia uhuru wake wa bendera, lilikazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa wananchi wa Zambia kujikita katika kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani; ukweli na umoja; udugu na usawa; daima wakitafuta mafao ya wengi. Zambia kwa sasa inajiandaa kwa ajili ya uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika hapo tarehe 20 Januari 2015 kufuatia kifo cha Rais Michael Chilufya Sata.

Tangu wakati huo, vyama vya kisiasa vimejikita katika kampeni ya kuomba ridhaa kutoka kwa wananchi, jambo ambalo mwanzoni lilianza kutishia amani, usalama na mustakabali wa taifa la Zambia. Wachunguzi wa mambo wanasema, watu wamesherehekea Noeli huku kampeni za uchaguzi mdogo zikiendelea kupamba moto!

Changamoto kubwa kwa sasa nchini Zambia ni mwendelezo wa umoja na mshikamano wa kitaifa uliojionesha katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, licha ya wananchi wa Zambia kusigana kwa maneno, lakini bado wameendelea kuwa wamoja, licha ya cheche za ufisadi kuanza kuchomoza wakati wa kampeni kwa kuoneshana ubabe wa fedha. Wanasiasa hawana budi kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, wanasaidia kupambana na umaskini wa hali na kipato nchini Zambia, kwa kutumia rasilimali iliyopo kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Hadi sasa kumekuwepo na malalamiko kwamba, utajiri na rasilimali ya nchi havijagawanywa sawa miongoni mwa wananchi wote!All the contents on this site are copyrighted ©.