2014-12-27 09:15:13

Dumisheni misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa! Matusi hayana tija!


Askofu Evaristo Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya, Tanzania, amewaasa wanasiasa nchini Tanzania kuacha dhana potofu ya kukiuka maadili mema kwa kutoa lugha za matusi majukwaani wakiamini kuwa ndiyo mwanasiasa bora katika jamii,jambo ambalo siyo kweli bali ni kukengeuka na kupotoka kimaadili. Ni wajibu wa vyama vya kisiasa kuhakikisha kwamba, vinajitahidi kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa, kwa ajili ya mafao ya watanzani wote, bila kuwakatisha watu tamaa kwa vurugu na kinzani zisizokuwa na mvuto wala mashiko!

Askofu Chengula aliyasema hayo wakati wa ibada ya mkesha wa Sikukuu ya Noeli, tarehe 24 Desemba 2014 uliofanyika katika Kanisa kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua, Parokia ya Mbeya mjini. Anasema viongozi wa Serikali na vyama vya siasa, wanatakiwa kuwaletea matumaini watanzania na kuwa kiongozi anayetukana wenzake katika majukwaa ya kisiasa, ni wazi kuwa hata naye akipata madaraka makubwa basi ataendelea kuwa hivyo, jambo ambalo siyo sahihi.

"Viongozi wetu wanatakiwa wamjue Yesu Kristo, ili wawe na roho ya kuleta matumaini kwa watanzania wote kwa kuhakikisha wanavunja utengano wa ukabila, udini, udugu ama eneo analotoka mtu ili watanzania wote waweze na furaha, upendo na mshikamano, kwa kusaidiana wakati war aha na shidaā€¯ anasema Askofu Chengula. Aliongeza kwa kuwataka watanzania kutimiza wajibu wao barabara kwa kuanzia katika ngazi ya mtu binafsi, familia na jamii kwa ujumla, ili kujenga na kuimarisha utamaduni wa haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati, hasa wakati huu watu wanapojikuta wakimezwa mno na utandawazi unaogubikwa katika ubinafsi.

Askofu Chengula akiangalisha kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Tanzania mwaka 2015, ameitaka Serikali kuangalia mfumo wa kuandikisha watu katika Daftari la kudumu la wapiga kura kwa kulifanyia maboresho zaidi, kwa kutoa muda wa kutosha, ili watanzania wenye sifa za kupiga na kupigiwa kura waweze kutumia vyema haki yao Kikatiba kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya taifa. Muda ukiwa finyu, watu wengi watajikuta wanashindwa kujiandikisha na hivyo kupoteza haki yao ya kushiriki katika demokrasia. Kasoro zilizojitokeza katika zoezi la kuandikisha wananchi katika Daftari la wapiga kura zifanyiwe maboresho zaidi, ili hata kura ya maoni kuhusu muswada wa Katiba Mpya inayopendekezwa, iweze kuwashirikisha watanzania wengi zaidi.

"Tunawaomba viongozi wetu watutengenezee njia ili kuufanya uchaguzi mkuu mwakani (2015), uweze kwenda vizuri zaidi" alisema Askofu Chengula.
Alisema kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita, watu walitembea katika giza kuu na walikaa katika ulimwengu wa kuonewa na kumwaga damu, lakini sasa wameona mwanga mkuu, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa kweli ni wajenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu.

Bado kuna vita, nyanyaso na madhulumu katika misingi ya kidini, mambo yanayowafanya baadhi ya watu kukosa haki yao ya kuwa na uhuru wa kuabudu. Hii ni changamoto kubwa kwa Serikali kuhakikisha kwamba, inazingatia utawala wa sheria na Katiba inatekelezwa kwa ajili ya mafao ya wengi. Chokochoko za kidini ni hatari kwa ustawi na maendeleo ya watu.

Yesu Kristo aliyezaliwa mjini Bethlehemu ni Mfalme wa haki na amani anayekuja kulifukuza giza katika maisha ya mwanadamu, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuhakikisha kwamba, wanaruhusu mwanga wa Kristo uweze kuwaangazia ili watembee katika upya wa maisha kwa kuachana na maisha ya kale yanayojikita katika dhambi na mauti! Noeli kiwe ni kipindi cha haki, amani, upendo na mshikamano, kwa kuwajali maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!
Na Thomposn Mpanji,
Mbeya, Tanzania.
All the contents on this site are copyrighted ©.