Askofu mkuu Carlos Osoro Sierra wa Jimbo kuu la Madrid, Hispania katika barua yake
ya kichungaji kwa ajili ya maadhimisho ya Siku kuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria
na Yosefu, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufanya tafakari ya
kina ili kuona uzuri na ukweli wa familia, mambo msingi yanayojikita katika moyo wa
kila mwanadamu. Itakumbukwa kwamba, Siku kuu ya Familia Takatifu inaadhimishwa tarehe
28 Desemba 2014.
Familia kama
Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambapo umoja na mshikamano katika maisha vinapaswa
kuwa ni sehemu ya vinasaba vyake; ni mahali ambapo zawadi ya uaminifu na udumifu katika
maisha ya ndoa na familia inachipuka na kuchukua sura yake katika maisha ya wanandoa.
Familia inaimarishwa kwa uwepo wa upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo, mwamba wa
tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.
Familia zikijijenga na kujisimika
katika mwamba ambao ni Yesu Kristo, kamwe hazitaweza kuyumbishwa katika maisha na
utume wake. Kutokana na ukweli huu, Injili ya Familia itaendelea kuwa ni Habari Njema
kwa ajili ya ulimwengu na chemchemi ya furaha kwa wengi, licha ya kinzani na changamoto
nyingi zinazoikumba familia kwa nyakati hizi.
Askofu mkuu Osoro anaialika
Familia ya Mungu Jimboni mwake, kuhakikisha kwamba, inaadhimisha Siku kuu ya Familia
Takatifu, kwa kuzionjesha familia zenye shida na mahangaiko makubwa, ile furaha, imani,
matumaini, mapendo na mshikamano wa dhati. Bado kuna familia ambazo zimeathirika vibaya
sana kutokana na myumbo wa uchumi kimataifa, hizi ni familia ambazo zinapaswa kuonjeshwa
umoja, mshikamano na upendo.
Askofu mkuu Osoro anazikumbusha familia umuhimu
wa kushiriki kikamilifu katika maisha ya Kisakrakenti kwa kupokea mara kwa mara Sakramenti
ya Ekaristi Takatifu na Kitubio, ili kweli Yesu aweze kupata nafasi katika maisha
yao ya kila siku. Anawaalika wanandoa watarajiwa kuhakikisha kwamba, wanajiandaa kikamilifu
kwa ajili ya kukumbatia na kuenzi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, tayari
kusaidiana katika hija ya maisha ili kufikia utakatifu na maisha ya uzima wa milele,
lengo kuu katika maisha ya Wakristo.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.