2014-12-26 10:36:01

Simameni imara katika imani, maadili na utu wema!


Watanzania wanaaswa kukitumia Kipindi cha Noeli kwa kuhakikisha kwamba wanadumisha amani, upendo na mshikamano na kamwe wasikubali, watu wachache wasiokuwa na nia njema na taifa wawagawe kwa misingi yoyote ile. Kauli hiyo imetolewa katika mkesha wa Sikukuu ya Noeli na Askofu mstaafu Mathias Isuja Josefu wa Jimbo Katoliki Dodoma wakati akiongoza Ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo wa msalaba, Jimboni Dodoma.

Askofu Isuja amewataka Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema kusherekea Sikukuu ya Noeli kwa kudumisha upendo na amani kwani hata Yesu Kristo alikuja duniani kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kumkirimia: furaha, amani na matumaini mapya.

Amesema kuwa sikukuu ya Noeli iwaunganisha watu wawe pamoja, washirikiane katika mambo yote lakini kwa namna ya pekee, kwa kuwasaidia masikini na wenye shida zaidi. Watanzania wametakiwa kuwa makini na utandawazi usiojali utu, heshima, upendo na mshikamano, kwani unaweza kuwatumbukiza katika majanga makubwa ya maisha. Baadhi ya watu katika jamii, wameathirika kutoka na utandawazi kwa kujiingiza katika biashara haramu ya binadamu, utumwa mamboleo, misimamo mikali ya kiimani; mambo ambayo yanahatarisha amani, ustawi na mustakabali wa Jumuiya ya Kimataifa.

Wakati huohuo Padre Dominiki Mwaluko akiongoza Ibada ya sikukuu ya Noeli katika Kigango cha Mtakatifu Maria de Mathias, kilichoko Jimbo Katoliki la Dodoma, amewataka Wakristo wawe ni watu wenye msimamo thabiti katika misingi ya imani, matumaini na mapendo, kwa kuendelea kuwa ni chachu ya amanim, utulivu na mshikamano unaofumbatwa kutoka katika undani wa maisha yao. Wakristo wawe ni chachu ya maisha adili na matakatifu, kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Waamini wajitahidi kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao, kwa kuachana na dhambi pamoja na nafasi zake.

Aidha kwa upande wa Parokia ya Kiwanja cha Ndege Jimbo Katoliki la Dodoma ambalo hivi karibuni limepandishwa hadhi na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Jimbo kuu, jumla ya watoto 120 wamebatizwa katika Siku kuu ya Noeli.


Katika mahubiri yake, Padre Sostenes Luyembe, SJ, amewataka wazazi kuendelea kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai, kwa kuhakikisha kwamba, wanawarithisha watoto wao imani, maadili na utu wema, daima wakionesha shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya watoto. Ujumbe wa Noeli anasema Padre Luyumbe unaopaswa kujikita katika mioyo na maisha ya watu ni kwamba, nyumba ya Kristo ni haki, amani na mapendo; nguzo msingi katika kuitegemeza familia ya mwanadamu.


Kwa upande wa waamini wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Damu Azizi ya Yesu, Kisasa Medelii, Jimbo Katoliki la Dodoma, Padre Parfect Leiya amewataka waamini kutumia Kipindi cha Noeli, ili kumwilisha upendo kwa Mungu na jirani zao, lakini zaidi kwa kuwajali maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Padre Leiya, Paroko wa Parokia hii amesema Noeli ni Sikukuu ya Familia inayojikita katika furaha, imani, matumaini, mapendo, huruma na faraja kwa kutoa nafasi ya pekee ili Yesu Mfalme wa amani na mshauri wa ajabu aweze kupata makao katika familia, ili kuziimarisha ziweze kuwa kweli ni shule ya utakatifu, haki, amani, msamaha na upatanisho, wakati huu Mama Kanisa anapojitahidi kutangaza Injili ya Familia kwa walimwengu!

Padre Leiya amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kutubu na kumwongokea Mungu kwa kutembea katika mwanga angavu unaoletwa na Mtoto Yesu. Ni mwaliko wa kuachana na matendo ya giza na kuambatana na Yesu, ambaye ni ukweli, njia na uzima.


Katika Kikanisa cha Kijiji cha Matumaini, Jimbo Katoliki Dodoma, kinachowahudumia watoto wanaoishi na virusi vya Ukimwi; Padre Vincenti Boselli, muasisi wa Kijiji hiki katika mahubiri yake wakati wa kuadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Stefano Shahidi, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Desemba, amewataka waamini kushuhudia imani, kuiadhimisha, kuimwilisha katika matendo adili na kuisali, kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji; imani ambayo Mtakatifu Stefano iliishuhudia hata mbele ya watesi wake, akawa tayari kujisadaka kwa ajili ya sifa na utukufu wa Kristo.

Mtakatifu Stefano aliitetea imani yake kwa matendo, akawa tayari kutoa msamaha hata kwa watesi wake, akifuata mfano wa Yesu mwenyewe aliyefundisha umuhimu wa msamaha hata alipokuwa ametundikwa pale juu Msalabani. Noeli, iwe ni Siku kuu ya kuonjeshana: huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwani kwa njia ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, Mungu ameingia katika historia ya maisha ya mwanadamu, ili kumkomboa kutoka katika dhambi na mauti, tayari kumshirikisha maisha ya uzima wa milele.

Zawadi kubwa wanayopaswa kuwaonjesha na kuwashirikisha wengine ni upendo, msamaha, imani na matumaini wale wote waliokata tamaa katika maisha yao, kwani Kristo aliyezaliwa ni sababu ya furaha, imani na matumaini.

Na Rodrick Minja,
Dodoma, Tanzania.
All the contents on this site are copyrighted ©.