2014-12-26 14:53:05

Kuweni na imani thabiti kama ya Mtakatifu Stefano ..Papa


Tarehe 26 Desemba, kwa mataifa mengi ni siku ya mapumziko, iliyopewa jina Boxing Day, ni Siku ya Kufungua vifushi vya zawadi ya Sikukuu ya Krismasi.
Katika Sikukuu hii, Baba Mtakatifu Francisko, nyakati za adhuhuri alijitokeza katika dirisha la Chumba chake cha kujisomea katika Jengo la Kipapa , na kutoa Neno kwa maelfu ya watu waliokuwa wamekusanyika katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro hapa Vatican, kusali pamoja naye sala ya Malaika wa Bwana.
Kwenye tafakari yake , Papa amerejea liturujia ya siku akisema, " wapendwa ndugu zangu, wake kwa waume, leo Liturujia inakumbuka ushuhuda wa Mtakatifu Stefano, ambaye alikuwa ni kati ya mashemasi saba wa kwanza, waliochaguliwa na Mitume, kwa ajili ya huduma ya upendo katika jamii ya Yerusalemu. Mtakatifu Stefano, Mkristo, shahidi wa kwanza wa Kanisa, kufia imani yake. Kuuawa kwake kama shahidi wa Ukristo, kwa kuyatoa maisha yake mwenyewe sadaka ya imani, kumemjengea heshima kubwa, katika ulimwengu wa Mfalme wa wafalme. Na hivyo inaonyesha wazi jinsi ya kuishi kikamilifu ndani ya siri hii ya Krismasi".
Papa Francisko ameendelea kutafakari Injili ya siku hii, akirejea hotuba ya Yesu kwa wanafunzi wake wakati akiwatuma kupeleka ujumbe akisema, “nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, ataokolewa "(Mt 10:22).
Papa amesema, maneno hayo ya Bwana, hayavurugi furaha ya maadhimisho ya Sikukuu ya Krismasi, bali yanaonya juu ya sherehe za uongo zisizokuwa na ukweli wala nia za adhimisho la Noeli. Ni maneno yanayotolewa kwa muumini, ili aweze kuelewa zaidi juu ya kipimo cha imani kinachokubalika katika maisha ya kawaida ya Kikristo kwamba, upendo hushinda vurugu, kifo huleta uzima. Papa aliongeza kusema kwamba, kwa kweli , kumkubali Yesu katika maisha, huongeza uwepo wa furaha ya Usiku Mtakatifu, na kutembea katika njia halisi iliyotajwa katika Injili hii, yaani, kumshuhudia Yesu kwa unyenyekevu, na katika hali ya kimyakimya, lakini bila hofu ya kwenda kinyume, wala kuumiza mtu mwingine. Papa alitoa mwaliko kwa waamini wote wa Kristo, kwamba, wameitwa kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Stefano, kuwa tayari hata kumwaga damu yao kwa ajili ya kutetea na kuikiri imani kwa Kristo.
Na aliendelea kuonya kwamba, kuifuta njia ya Injili , kwa hakika ni mchakato katika uthabiti wa moyo. Kwa wale ambao hutembea pamoja kwa uaminifu na ujasiri, hupata zawadi ya ahadi iliyotolewa na Bwana kwa watu wote, wake kwa waume wenye mapenzi mema. Papa alieleza na kurejea tukio la kuzaliwa kwa Bwana Bethlehem, ambako Ukweli ulitangazwa na malaika kwa wachungaji: "Amani duniani , kati ya wamchao Mungu (Lk 2:14). Hii ni amani inayotolewa na Mungu, yenye uwezo wa kuongoza dhamiri hata inapobidi kupita katika njia ya majaribio ya maisha, hasa kwa wale ambayo tayari wamepokea na kukubali kuongozwa na Neno la Mungu na kujitahidi kudumu nalo kwa uvumilivu mpaka mwisho (Mat 10:22).
Papa alieleza na kuwakumbuka kwa namna ya pekee, wale wanao wanaopambana na kubaguliwa kwa ajili ya ushuhuda wao kwa Kristo. Alimtia shime kila mmoja wao, kuubeba msalaba wa mateso hayo kwa upendo, hadi kuingia ndani ya fumbo kamili na Noeli, katika moyo wa Kristo na Kanisa.
Papa aliendelea kuomba sala za shukrani pia kwa sadaka ya mashahidi hawa leo ambao ni msaada mkubwa katika kuimarisha utambulisho na kazi zinazo tafuta haki kwa ajili ya uhuru wa kidini sehemu zote za dunia, haki isiyoweza hamishika kwa kila binadamu.
Papa aliwatakia wote mapumziko mema kwa nyakati hizi za Siku Kuu ya Krismasi akiwataka wote waige imani ya Mtakatifu Stefano, shemasi na mfiadini wa kwanza, wakati wanapo endelee kutembea pamoja kama waamini wa Kristo, katika njia yao ya maisha ya kila siku, kwa matarajio ya kuvalishwa taji l aushindi, katika siku ya mwisho, wakati wa sherehe kubwa ya kukutana na Watakatifu katika Paradiso.
Na alihitimisha hotuba yake na salamu za furaha ya Krismasi na mwaka mpya, kwa wote waliokuwa wakimsikiliza, kwa wao wenyewe na kwa familia zao,pia kwa Parokia, jumuiya za kidini na vyama vya kikanisa, aliwaombea Malipo mazuri kutoka kwa Bwana wa Ukarimu.
All the contents on this site are copyrighted ©.