Jengeni umoja na mshikamano unaojikita katika uwajibikaji; utu na heshima ya binadamu!
Mfalme Abdullah wa Pili wa Yordan, katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli, amewatumia
salam na matashi mema Wakristo wote nchini mwake na kuwatakia kheri na fanaka kwa
Mwaka Mpya wa 2015. Katika salam zake, Mfalme Abdullah wa Pili anawataka waamini na
wananchi wote kwa ujumla kushikamana ili kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa; kuendeleza
uzalendo unaofumbatwa katika uwajibikaji na mshikamano wa kijumuiya!
Kuna mabadiliko
makubwa yanayoendelea kutokea katika ulimwengu wa utandawazi, baadhi ya mabadiliko
haya yanaonesha ustawi na maendeleo kwa binadamu, lakini baadhi yake yanatia shaka
na wasi wasi mkubwa kuhusu hatima na mustakabali wa maisha ya mwanadamu kwa siku za
usoni. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene,
ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu, kwa kuthamini hata tofauti
zinazojitokeza kati ya watu.
Viongozi wa kidini nchini Yordan wanaendelea kukazia
umuhimu wa wananchi kushikamana na kusaidiana ili kudumisha umoja wa kitaifa, pamoja
na kuendelea kuwa ni nchi ya mfano kwa Waislam na Wakristo kuishi kwa amani na utulivu,
licha ya tofauti zao za kidini na kiimani. Yordan imekuwa ni bandari ya salama na
matumaini kwa watu wanaokimbia vita, nyanyaso na madhulumu ya kidini huko Mashariki
ya Kati.
Wakimbizi na wahamiaji wanalipongeza Shirika la Misaada la Kanisa
Katoliki, Caritas Yordan kwa kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kwa upendo na uvumilivu
mkubwa, kiasi kwamba, watu wamefanikiwa kupata makazi, chakula na mahali salama zaidi
kwa familia zao!