Leo ni Sikukuu ya Familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Katika sikukuu hii tunapata
masomo ya kumtolea Yesu hekaluni. Katika kanisa la mashariki sikukuu ya kumtolea Yesu
hekaluni inaitwa "hypapante" yaani Sikukuu ya kukutana, au sikukuu ya
maonano.
Katika Sikukuu hii, Mwinjili Luka anatuletea “hypapante”
au maonano mbalimbali yanayoweza kujieleza kitaalimungu zaidi kuliko kihistoria. Mathalani,
Yesu alisema: “Libomoeni hekalu hili nami nitalijenga kwa siku tatu, Hekalu lililo
na maana ya nafsi yake mwenyewe. Kwa hiyo mkutano wa kwanza ni ule wa hekalu hai la
Agano Jipya yaani Yesu Kristo mwenyewe au Wakristu, na Yerusalem hekalu la Agano la
Kale au waisraeli.
Halafu Yesu ni Neno umbaji la Mungu aliyefanyika mwili
(Neno la Agano jipya). Kadhalika ndani ya hekaluni kuliwekwa Torah, yaani Neno umbaji
la Mungu la Agano la Kale. Kwa hiyo, mkutano wa pili ni kati ya Neno la Agano Jipya
na Torah. Kuna pia kukutana kwa binadamu Yesu na binadamu wenzake waliokusanyika Yerusalemu.
Lakini katika mkutaniko huo ni watu wawili tu walioweza kumtambua Yesu kuwa binadamu
wa pekee. Watu hao ni mzee Simoni, na bibi Anna binti Fanuel wa kabila la Asher. Watu
hawa wanafurahia kumtambua na kumshika na kumkumbatia Mungu aliyejifanya binadamu
kama wao.
Tunajulishwa wazazi Yosefu na Maria waliofika hekaluni na sadaka
zao nyonge: “Hua wawili au makinda ya njiwa wawili.” (Lk. 7:22-23). Kwa kitendo cha
wazazi hao tunapata ujumbe wa kujifunza. Mosi wazazi hawa wanatufundisha kuwa kila
mtoto ni mali ya Mungu, wao wamekabidhiwa mtoto wamwandae ili aweze kuishi wito wake
alioumbiwa hapa duniani, yaani wamsaidie mtoto wao atimilize ndoto aliyo nayo Mungu
kwa huyo mtoto.
Aidha kila mtoto anayezaliwa duniani ni zawadi ya upendo itokayo
kwa Mungu kwa ajili ya ulimwengu na kwa binadamu wenzake. Kwa hiyo wazazi wasijimilikishe
mtoto huyo na kumkandamiza bali wamtolee Mungu. Aidha, wazazi wanatolea hekaluni njiwa
wawili, alama ya ufukara ni tofauti na utajiri wa zawadi ya Mungu anayoupatia ulimwenguni.
Baada
ya kutoa sadaka sasa wanaonana na wazee wawili Simoni na Anna. Hao wanawakilisha watu
wa Agano Kale waliongojea ujio wa Agano jipya. Yesu alikuwa ni mmojawapo kati ya watoto
wengi waliofika kutolewa hekaluni. Kulikoni ni watu wawili tu Simoni na Anna wanaofaulu
kumtambua mtoto huyu kuwa ni masiha.
Injili yatuambia kuwa mwenye moyo safi
ndiye atakayemwona Mungu. Simoni alikuwa “mtu wa haki na mwenye moyo safi.” Kutokana
na usafi wake wa moyo, Simoni anafaulu kuona hadhi na sifa ya pekee ya mtoto kwa macho
tofauti na wanavyoona wengine. Aidha Simoni alikuwa na “roho wa Mungu ndani yake.”
Huyo roho wa Mungu ndiye aliyemwangazia kuwa asingeona kifo bila ya kumwona Masiha.
Kwa njia ya roho wa Mungu Simoni hakuchanganyikiwa na kuvurugwa na mizengwe ya ulimwengu
huu.
Sisi kama hatuvurugiki, hatuchafui sauti hii kwa namna yetu ya kuishi
na kufikiri, huyo roho anaweza pia kuongea nasi na kutushuhudia. Tujitahidi kumwona
roho katika neno lake, katika jumuiya, katika wale wanaoshuhudia Ufalme wa Mungu katika
maisha yao, na tutaweza kuigundua sauti ya Bwana.
Kwa vile Simeoni alimsikiliza
roho huyo akaweza kumsifu Mungu kwa sababu Mungu amempa utambuzi wa umaana wa maisha
yake. Ndiyo maana sasa anasali: “Sasa Ee Bwana wamruhusu mtumishi wake anaenda sehemu
ya amani, kwani macho yangu yameona wokovu…” Huyo mzee anatufundisha jinsi ya kuzeeka
vizuri. Hatazami nyuma bali mbele.
Kwake yeye kifo kinaleta maana ya maisha
yote. Kifo ni hatima ya maisha yaliyokuwa na maana kwani kwa vile yalikuwa daima yanaongozwa
na roho. Simeon, analiacha pazia la ulimwengu huu na kuelekea kwenye amani “sasa ni
wakati wangu wa kuacha pazia la imani”( Paulo kwa Timoteo). Simeoni baada ya kuona
na kushuhudia yote sasa hajifikirii tena mwenyewe, bali anawafikiria watu wote kwamba
sasa wamepata wokovu. Ameona mwanga na sasa kwa amani anaenda kupelekea habari njema
aliyoiona kwa wale wote waliozaliwa kabla yake na hawakuona huo mwanga. Watu hao ni
akina Adamu na Eva, Abrahamu, Isaka, Yakobo na wengineo.
Kisha anawabariki
Maria na Yosefu na kutabiri: “Yeye ni ishara ya kuanguka na kufufuka kwa wote katika
israeli, na alama ya ukinzani, nawe upanga utakupenya”. Mara nyingi unabii juu ya
upanga utakaompenya Maria unaunganishwa na uchungu wa Maria aliposimama chini ya msalaba
wa mwanae. Ufasiri huo ni potovu, kwani kazi ya upanga uliotajwa hapa ni kukata na
kutenganisha pande mbili kitu kinachokatwa.
Kutokana na wito wa kuushuhudia
alio nao mtoto huyu kwa ulimwengu, watu wengine wa ulimwenguni watampokea na wengine
watamkataa. Kwa hiyo upanga utakaomchoma Maria anayewakilisha taifa la Israeli ni
uchungu utakaowasibu kwa vile wengine kati yao hawatampokea Masiha.
Kwamba
wachache watamtambua (watampokea) na wengi hawatamtambua (watamkana). Hata kwa Maria
binafsi alijihisi kugawanyika katika safari yake ya imani, kwa vile mambo mengine
ya Kristu aliyaelewa mengine hakuyaelewa: “Wazazi wake hawakuelewa waliyoambiwa lakini
wakayaweka yote moyoni.” Kadhalika mgawanyiko huo uliwakumba pia mitume wake. Mama
Bikira Maria anaitwa mbarikiwa, kwani alikuwa daima kati ya mitume waliokuwa katika
sala, wakilisikiliza Neno la Mungu na kulishika.
Kuhusu Nabii wa kike Anna,
binti Fanuel wa kabila la Asher. Kabila linalomaanisha mbarikiwa. Lilijiingiza mno
katika utajiri wa watu wa mahali walipokuwa kisha likafifia lote. Mama huyu wa miaka
84, aliishi miaka 7 tu na mume wake kisha akabaki mjane mwaminifu kwa miaka mingi
bila kuolewa tena. Nambari hiyo ni alama ya ukamilifu ukizidisha namba mbili kamilifu
7 mara 12.
Mwanamke huyu ndiye anayempokea Bwana arusi Masiha Yesu Kristu.
Ni ngumu kumpokea Mungu na ni ngumu zaidi kuishi kidhati maisha ya imani kwa Kristu.
Tukiwa na moyo safi, tukiongozwa na roho wa Mungu (Kristu) na kudumu tutaweza kumtambua
Mungu katika maisha na kumwishi daima.