Mpendwa mwana wa Mungu, leo tunasherehekea na kushangilia sherehe ya familia Takatifu.
Masiha amezaliwa ndani ya familia hii. Ndani ya familia hii kuna majukumu ya kutekeleza
ili Mwana wa Mungu akae mahali stahili na kwa namna hiyo atufundisha namna ya kutenda
na kuishi kwenye familia zetu.
Somo la kwanza
toka kitabu cha Hekima ya Yoshua bin Sira linaweka mbele yetu fahari na heri ya kuwaheshimu
wazazi na kuwatunza katika uzee wao. Heri ambazo ziko wazi kadiri ya somo hili ni
kuwa na uzao, na si uzao tu bali kufurahia uzao huo. Kuwa na maisha marefu na uzee
wa kusifika. Kwa kuwatunza wazazi na kuwapa heshima stahili mmoja afanya malipizi
ya dhambi zake. Kwa hakika somo hili lasisitiza na kuweka mkazo juu ya amri ya nne
ya Mungu. Waheshimu baba na mama upate miaka mingi na heri duniani.
Mtakatifu
Paulo anapowaandikia Wakolosai anafafanua namna ya kuishi na kupendana katika familia.
Ameweka wazi fadhila ambazo zajenga maisha ya familia yaani, unyenyekevu, utu wema,
rehema na msamaha kwa kila mwanafamilia. Kilainisho cha fadhila hizi ni UPENDO kifungo
cha ukamilifu. Kama familia na hasa kila mwanafamilia ataweza kuitikia mwaliko huu
wa Mungu, basi familia nzima itakaa katika utulivu na amani ya kweli, yaani inayokuza
mshikamano.
Mtume Paulo haishii tu kwenye kusema upendo bila kuweka jambo
la kuishi upendo huo, yaani kusikia na kusikiliza sauti ya Mungu kwa njia ya Neno
la Mungu. Kwa kutafakari Neno la Mungu tunajiweka tayari siku zote kukaa na Bwana
aliye Neno wa Milele, aliye nuru angavu tuliyoipokea wakati wa siku ya Noeli. Kwa
hakika ni kukaa na Bwana aliye Neno lenyewe (Yn 1:1-).
Pamoja na fadhila
nyingine, fadhila ya utii yatufaa kwanza kwa kutii Neno la Mungu na pili kutii mamlaka
iliyowekwa na Kristo katika familia. Baba ni mkuu wa familia yafaa kumtiii na kumheshimu
lakini yeye mwenyewe lazima aige mfano wa Kristo Mchungaji mwema anayewahangaikia
kondoo wake. Ndiyo kusema aoneshe daima fadhila ya upendo kwa mke wake, watoto wake
na watu wote.
Katika Injili ya Luka tunapata mfano wa familia iliyo na
utii kwa sheria za kidini. Ni lazima wakampeleke mzaliwa wa kwanza hekaluni. Yesu
Mwana wa Mungu atufundisha kujitoa kabisa kwa Mungu anayetuagiza daima kutimiza mapenzi
yake kwa njia ya Kanisa. Kwa kumpeleka Yesu Kristu huko hekaluni wanaonesha pia wajibu
wa kumwelisha mtoto katika elimu ya dini na wajibu kijamii. Ndiyo kusema wewe mzazi
unapaswa na unawajibika kutoa mafundisho msingi ya kikristu na unawajibika kutafuta
shule itakayomkuza mwanao vema katika utu, ukristu na malezi kijamii.
Jambo
jingine tunaloliona katika Injili ni lile la Simeoni kumchukua mtoto Yesu toka mikono
ya wazazi wake, na baadaye kumtoa kwa watu wote. Kwa jambo hili Simeon anawakilisha
taifa la Israeli lililokuwa likisubiri ujio wa Masiha, na sasa amefika na kumtoa kwa
wote maana yake Masiha si wa Israeli tu, bali ni kwa ajili ya mataifa. Simeon katika
maisha yake alikuwa akisubiri bila manunguniko, ni alama ya wazee wa sasa ambao wanajikabidhi
mikononi mwa Mungu, wakisali na kuimba daima, na kungojea fadhili za Bwana huku wakitimiza
wajibu wao wa kujenga hekima katikati ya familia zao na watu.
Katikia
Injili hiyo ya Luka, tunaona pia, binti mwanamke aitwaye Anna, huyu ni mfano wa unyenyekevu
na uwajibikaji katika kutimiza kazi ya Bwana. Ni mfano wa wale ambao wametayarisha
njia ya Bwana na mapito yake. Anatoka katika ukoo mdogo wa Asheri ambao mbele ya Waisraeli
ni bure na maskini, lakini toka hapo Anna anampokea Bwana kwa furaha. Hii ni habari
ya furaha kwako wewe mwamini katika udogo wako na utauwa wako, yakwamba daima kuna
matunda makubwa ya neema za Mungu atika upole na unyenyekevu.
Hawa tuliowasikia
katika Injili wakitenda kazi ya Bwana, wanakuwa kichocheo cha wanafamilia kutenda
vema katika familia zao, daima wakilenga utukufu wa Kristo uliokwishafunuliwa kwetu
na Bwana mwenyewe.
Ninakutakieni heri tele wewe uliyemdau wa familia na hasa
unapoweka nguvu yako kukuza tunu bora za familia, ukiangazwa na familia takatifu ya
Yesu, Maria na Yosefu. Heri tena kwa jumuiya zote, parokia zote, mashirika ya kitawa
mliojiweka chini ya usimamizi na ulinzi wa familia takatifu. Tumsifu Yesu Kristo Maria
na Yosefu.
Tafakari hii inakuja kwako toka Padre Richard Tiganya, C.PP.S.