Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO linasema kwamba, ugonjwa wa
Ebola unaendelea kutishia usalama wa maisha ya wananchi wengi Afrika Magharibi na
kwamba, kuna watu zaidi ya millioni moja wanaotishwa na baa la njaa kutokana na janga
lililosababishwa na ugonjwa huu.
Hii inatokana na baadhi ya nchi jirani kuamua
kufunga mipaka ya nchi zao kwa kuhofia maambukizi ya ugonjwa wa Ebola kutoka katika
maeneo yaliyoathirika zaidi, hali ambayo imepelekea pia myumbo wa uchumi katika nchi
kadhaa huko Afrika Magharibi. FAO na Mpango cha Chakula wa Umoja wa Mataifa, unaitaka
Jumuiya ya Kimataifa kuunganisha nguvu, ili kuokoa maisha ya maelfu ya watu huko Afrika
Magharibi, wanaokabiliwa na baa la njaa!
Baraza la Maaskofu Katoliki Sierra
Leone, linawaomba waamini pamoja na wasamaria wema kuguswa na mahangaiko ya wananchi
walioathirika kutokana na ugonjwa wa Ebola kwa kuchangia kwa hali na mali, ili kusaidia
huduma zinazotolewa na Kanisa kwa waathirika wa janga la Ebola. Vituo vya afya vinavyomilikiwa
na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Sierra Leone kwa sasa vinahitaji msaada mkubwa,
ili kuviwezesha kutekeleza utume wake, vinginevyo, hali itakuwa ni mbaya zaidi, si
tu kwa sababu ya ugonjwa wa Ebola, bali kwa kutambua kwamba, hata magonjwa mengine
nyemelezi yanaendelea kushika kasi kutokana na hofu ya kuambukizwa ugonjwa wa Ebola.
Ebola ni ugonjwa ambao kwa sasa unatishia mshikamano na mfungamano wa kimataifa!