2014-12-25 10:28:11

"Tafadhali, nitunzie siri!


Leo ni siku ya furaha. Tunapokutana tunatakiana “Merry Christmas” na kupeana zawadi. Nami zaidi ya kukutakia heri ya christmas, ninapenda pia kukupatia zawadi ya Krismasi. Lakini naomba nikutonye kabla, kwamba zawadi hiyo ni siri. Ingawaje waswahili wanasema “hakuna siri ya watu wawili,” ninakutahadharisha kuwa, pale utakapowalopokea pengine hawatakuamini au wanaweza wakakuelewa vibaya.


Siri yenyewe ni kwamba “Umebahatika sana kuwa na imani,” tena “imani kwa nafsi iliyo hai, ambayo ni Kristo mwenyewe Mwana wa Mungu aliye hai.” Nafsi hiyo siyo ukweli wa kufikirika ulioandikwa kwenye msaafu, bali ni nafsi halisi, iliyo uzima na ni mwongozo unaokupeleka kwenye utimilifu wa maisha ya furaha kwanza, ya hapahapa duniani, halafu furaha ya mbinguni. Waswahili wanasema: “Bahati ina miujiza, lakini haina ahadi.” Nafsi hiyo iliyo halisi, uzima na mwongozo unaiona katika sikukuu ya leo.


Muujiza mmojawapo ni kule kuwezeshwa kuelewa mambo ambayo wasio na imani hiyo hawawezi kamwe kuyaelewa. Wewe umebahatika kujua maana ya mambo yatokeayo na kuweza tafsiri ya matendo ya kawaida ya maisha wanayofanya watu. Hakika unaweza kusoma ishara za nyakati na kutambua maana ya matendo yafanyikayo katika ulimwengu wa kisiasa, ulimwengu wa dini, wa mambo ya familia na hata kuyatafsiri matatizo yako binafsi.


Nitakupa mfano unaohusu sikukuu ya leo. Unashuhudia mwenyewe jinsi watu walivyohamasika kuandaa na kusherekea krismas. Wanavyokula mapochopocho, wanatia viwalo vya pekee na kufurahi sana. Mataifa mengine kama vile Wajerumani wa kusini leo wanakula keki maalumu ya Noeli inayoitwa Lebkuchen, na keki ya waitalia inaitwa panettone. Kadhalika leo kuna kuvaa nguo za pekee za sikukuu. Watu wote tunavifurahia vyakula na viwalo hivyo, lakini ni bahati ya walio na imani kwa Kristu tu ndiyo wanaofahamu kwa nini wanafanya hivyo. Wengine wote ni ushabiki tu wa kula na kunywa basi, na pengine sanasana wanajua sikukuu hizi ni za kufanya vizuri biashara zao.


Mfano mwingine, ulitokea miaka kumi na nne iliyopita, pale jinsi watu walivyoisubiri na kuishangilia Millenia mpya ya tatu. Ingawaje wote tuliona fahari kuwaona watu wote dunia wakiisherekea miaka hiyo, lakini kwako wewe mkristu hukufurahia tu kule kubadilika kwa tarehe na kuwa miaka 2000, bali sikukuu hiyo kwako ilieleweka vizuri zaidi, kwamba ulikuwa ni ukumbusho wa mwanzo wa historia mpya na ya pekee ya dunia, miaka elfu mbili toka kuzaliwa Kristo.


Utaigundua zaidi bahati uliyo nayo, pale utakapokutana na mtu asiye na imani anapokabiliwa na matatizo mazito ya maisha anavyohaha na kukata tamaa. Alama ya kukata tamaa unaiona jinsi anavyoyakabili matatizo yake, akitumia nguvu na kudhulumu asijue anaongeza tatizo juu ya tatizo. Mtu huyo ameikosa nafsi hai ya kuilalamikia na ya kujadiliana nayo matatizo yake.


Kumbe, wewe umebahatika kuwa na nafsi hai ambayo ni Kristu aliyezaliwa, aliyekua, aliyeteswa na kuuawa lakini akafufuka. Hivi kudhulumiwa kwake, mateso na kifo chake vyote vinapata mwanya au nafasi ya kuwa na amani na upendo, hatimaye ni kuwa na furaha katika mateso. Unaona bahati uliyo nayo, kwamba katika matatizo, katika madhulumu na kuonewa, wewe unabaki kuwa na furaha, amani na upendo.


Ndugu yangu, binadamu wa leo siyo kwamba hana imani, la hasha, anayo imani, tena imani kubwa sana. Watu wengine wanayo imani kubwa kukushinda wewe unayejidhani unayo imani ya msimamo mkali wa dini yako. Angalia wenzako walivyo na imani kwa matangazo ya biashara, matangazo ya vipodozi vya urembo, matangazo ya dawa za kuongeza ukubwa wa maumbile, kuna imani juu ya chama cha siasa na sera zake hata kama zinatuongoza porini au zinazamisha jahazi. Kuna watu wana imani kubwa sana kwa maagizo ya mganga wa kienyeji hata wakikuagiza kuua.


Tofauti iliyopo kati ya imani zao na yako ni kwamba, imani ya mkristu imejengwa katika Mungu aliye nasi “Emmanuel”. Huyo ni Mungu aliye hai, Mungu mwema na mwenye haki, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristu. Kama alivyopenda kusema Paulo mtume: “Utaonanana naye huyo Mungu unapoonana na Yesu wa Nazareti.” Hakuna aliyemwona Baba ila Mwana… na yule ambaye Mwana apenda kumfunulia.” (Mt. 11:27).


Tofauti nyingine ni kwamba wewe uliye na imani kwa nafsi hai ya Kristu, unakuwa huru. Hakuna kitakachokutisha, hakuna kutishwa na masherti ya mganga, wala mateso, wala kifo. “Mkishika neno langu katika neno langu, ninyi ni wanafunzi wangu; mtauelewa ukweli, nao ukweli utawaweka huru” (Yo. 8:31-32). Kwa hiyo “Pale alipo Roho wa Bwana, hapo pana uhuru” (2Kor. 3:17).


Tofauti nyingine ni kwamba wewe umebahatika kujua maana ya sherehe ya leo kuwa sikukuu hii siyo ukumbuko, bali ni sherehe za utimilifu wa unabii. Unabii uliokuwa ni sauti ya maandamano ya mgomo dhidi ya mambo ya ulimwengu huu, dhidi ya kuonewa, dhidi ya ubabe. Ubabe huo unadokezwa mwanzoni tu mwa Injili ya usiku wa Noeli lilipopitishwa tangazo la kiubabe: “Kukatokea tangazo toka kwa Kaisari Augusto la kuhesabu watu wote duniani.” Kuhesabu watu maana yake watu walio nafsi hai, wanashushwa hadhi hadi kufikia kiwango cha kuwa bidhaa inayoweza kuhesabiwa. Binadamu hujulikani kwa jina bali kwa nambari, hiyo ndiyo senza.


Wakati huo watu wanapodhalilishwa hivyo ndipo mtoto anazaliwa. HapoMungu anaianzisha historia mpya Betlehemu, pahala palipokuwa pa mwisho kabisa duniani, tena anazaliwa kizizini na anajionesha kwa wachungaji watu wanyonge wa mwisho, na anakubali kuzaliwa na kulelewa na binti mdogo na mnyonge Maria.


Ndugu yangu, ni wewe peke yako unaposherekea Noeli hii ndiye unayeweza kujua mtoto huyu ataishije na ataishia wapi. Ukiijua siri hiyo utaweza pia kutambua sherehe za leo zinataka kutufundisha nini katika maisha yetu. Aidha, utaelewa pia maana ya kusherekea hata sikukuu ya kuzaliwa kwako na maisha yako yalivyo na hatima yake. Siri niliyokupa unaweza kuigundua vizuri zaidi kuwa ni siri iliyo wazi pale utakapouangalia uso wa mama baada tu ya kujifungua mtoto wake.


Furaha aliyo nayo baada ya uchungu mkuu wa kujifungua, hiyo inakuwa ni siri yake mwenyewe. Nadhani hata malaika walipoyaangalia macho ya Maria baada ya kujifungua mtoto Yesu hawakuelewa kitu. Pengine hata Maria mwenyewe ingawa alifurahi lakini hakuelewa sana maana ya uzao ule, hasa tunaposikia kwamba “akayaweka yote moyoni mwake, akiyatafakari.” Ila kwa uhakika maana halisi ya noeli alikuja kuifahamu alipokuwa chini ya msalaba. Nawe utatambua zaidi maana ya Noeli yatakapokupata. Naomba unitunzie siri, na Heri sana kwa sikukuu ya Noeli.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.
All the contents on this site are copyrighted ©.