Mwanga angavu wa Mtoto Yesu uvunjilie mbali giza katika mioyo ya watu!
Watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu; wale waliokaa katika nchi ya uvuli
wa mauti, nuru imewaangazia. Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, utukufu wa Bwana
ukawang’aria pande zote.
Hivi ndivyo
Liturujia ya Neno la Mungu inavyosikika wakati wa kesha la Siku kuu ya Noeli, yaani
kuzaliwa kwa Mkombozi, asili ya mwanga unaopenya na kuondoa giza. Uwepo wa Yesu Kristo
miongoni mwa watu wake unaondoa uzito wa kushindwa na huzuni ya utumwa na hivyo kuwakirimia
tena watu furaha.
Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Francisko alivyosema wakati wa
mahubiri yake, kwenye Ibada ya Misa Takatifu, Kesha la Noeli, iliyofanyika kwenye
Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Anasema, hata waamini wakati wa mkesha
huu wamekuja Nyumbani kwa Bwana kwa kupitia kwenye giza linaloifunika dunia, lakini
kwa kuongozwa na mwanga wa imani unaoangazia mapito yao, wakiwa wamejazwa na matumaini
ya kukutana na mwanga mkuu. Kwa waamini kufungua mioyo yao, wanauwezekano wa kutafakari
muujiza wa Mtoto mwenye nuru inayoangaza mawio kutoka juu.
Baba Mtakatifu anasema,
giza limeendelea kumwandama mwanadamu katika historia ya maisha yake tangu siku ile
Kaini alipomwaga damu ya ndugu yake Abeli kutokana na wivu usiokuwa na mashiko, mauaji,
vita, chuki, uhasama na kinzani zimeendelea kusikika katika uso wa dunia. Lakini kwa
subira na unyenyekevu mkuu, Mwenyezi Mungu ameendelea kumsubiri kwa uaminifu na uvumilivu
mkuu mwanadamu aliyemuumba kwa sura na mfano wake, licha ya mwanadamu kukengeuka.
Katika
historia, mwanga unaofukuza giza umeonesha kwamba, Mwenyezi Mungu ni Baba mwenye uvumilivu
unaojikita katika uaminifu kiasi cha kushinda giza na uasi wa mwanadamu, kiini cha
Habari Njema katika kesha la Noeli. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na uvumilivu,
anayevuta subira, kama ilivyokuwa kwa Baba mwenyehuruma, alipokuwa anamngojea Mwana
mpotevu, ili aweze kurejea tena nyumbani.
Baba Mtakatifu anasema, Nabii Isaya
anatabiri kwamba, Mwanga angavu utavunja giza na Mtoto Yesu anazaliwa na kupokelewa
kwenye mikono pendelevu ya Bikira Maria na upendo kutoka kwa Mtakatifu Yosefu pamoja
na mshangao wa wachungaji kutoka kondeni. Ni mtoto aliyelazwa kwenye pango la kulishia
wanyama, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo na unyenyekevu wa Mwenyezi Mungu,
aliyejitwalia unyonge, mateso, mahangaiko, matarajio na mipaka ya mwanadamu. Mwanadamu
kutoka katika undani wa maisha yake, alikuwa anatafuta faraja ya Mungu anayemwangalia
kwa jicho pendelevu, anayekubali mapungufu ya mwanadamu na kuridhika na udogo wake.
Baba
Mtakatifu Francisko anawaalika waamini katika mkesha wa Noeli, kujiuliza ikiwa kama
kweli, wamefanikiwa kuipokea huruma ya Mungu, kwa kumwachia nafasi, ili aweze kuwafikia
au wamekuwa ni kikwazo? Lakini jambo la msingi kwa waamini kumwachia nafasi Mwenyezi
Mungu ili aweze kumtafuta ili aweze kumbembeleza kwa upendo pamoja na kujiuliza swali
la msingi, ikiwa kama kweli waamini wanampenda Mwenyezi Mungu.
Baba Mtakatifu
Francisko anaendelea kuwahoji waamini, ikiwa kama bado wana ujasiri wa kupokea kwa
wema magumu na mateso yanayowazunguka katika maisha au pengine wameamua kuchukua njia
ya mkato, isiyofumbata tunu msingi za Kiinjili? Baba Mtakatifu anasema, dunia hii
inahitaji huruma ya Mungu. Changamoto za maisha hazina budi kukabiliwa kwa njia ya
wema na upole, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amejinyenyekesha na kujifanya kuwa
mdogo, ili aweze kukutana vyema zaidi na binadamu.
Huu ni mwaliko wa kumfungulia
mioyo yao, kwa kumwomba ili aweze kuwasaidia kuwa kama alivyo, awajalie neema ya upole
wanapokabiliana na changamoto pamoja na magumu katika maisha; awajalie kuonja ukarimu
wakati wa shida na uvumilivu wakati wa kinzani.
Baba Mtaakatifu Francisko anahitimisha
mahubiri yake kwa kusema kwamba, waamini katika kesha la Siku kuu ya Noeli, wanatafakari
mwanga angavu, ulioonekana na watu wa kawaida kabisa, wale ambao walikuwa wamejiandaa
kwa ajili ya kupokea zawadi ya Mungu. Tofauti kabisa na watu waliokuwa na kiburi pamoja
na majivuno; wale wanaotunga sheria kwa ajili ya mafao yao binafsi; watu wanaojifungia
katika ubinafsi wao. Waamini wanapoangalia Pango la Mtoto Yesu, wamwombe Bikira Maria
ili awawezeshe kumwona Mtoto Yesu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.