2014-12-25 11:31:18

Matashi mema ya Noeli kwa Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli na Mwaka mpya wa 2015 anaendelea kupokea salam na matashi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Watoto wagonjwa pamoja na familia zao wanaotibiwa kwenye Zahanati ya Mtakatifu Martha, iliyoko mjini Vatican, iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II ili kutoa huduma kwa maskini, Jumatano, tarehe 24 Desemba 2014, walikutana na kusalimiana na Baba Mtakatifu Francisko, ili kumtakia kheri na matashi mema katika Siku kuu ya Noeli na Mwaka Mpya 2015.

Watoto wanamwombea Baba Mtakatifu tunza na ulinzi kutoka kwa Mwenyezi Mungu; wazazi wanashukuru kwa huduma bora wanayopita kutoka kwa madaktari na wauguzi wa Zahanati hii inayohudumia watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia bila ubaguzi, ili kuwaonjesha wote huruma na upendo wa Mungu. Wazazi wanamshukuru Baba Mtakatifu kwa maneno na ujumbe wake unaogusa sakafu za mioyo ya waamini, kiasi cha kuwatia ari na moyo wa kusonga mbele, licha ya magumu na changamoto wanazokabiliana nazo.

Baadhi ya wazazi wanasema katika salam zao za Noeli kwa Baba Mtakatifu Francisko, kwamba, wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa uwepo na utume wake kwa Kanisa wakati huu! Wanamwombea kwa Mwenyezi Mungu, ili aendelee kuwatangazia watu wa Mataifa Injili ya Furaha na Matumaini, kwa wale waliokata tamaa na kupondeka moyo. Wanampongeza Baba Mtakatifu kwa ujasiri na unyenyekevu wake; wanamwombea hekima, afya ya roho na mwili, aendelee kujenga Ufalme wa Mungu, unaojikita katika misingi ya: haki, amani, upendo, utu na heshima ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.