2014-12-25 12:48:49

Kilio cha damu ya watu wasiokuwa na hatia duniani!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Siku kuu ya Noeli, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, alipanda kwenye ghorofa ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwa ajili ya kutoa salam za Noeli na Baraka kwa ajili ya mji wa Roma na Dunia kama zinavyojulikana kwa lugha ya Kilatini, “Urbi et Orbi”, tukio ambalo limehudhuriwa na maelfu ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia na wengine wengi waliofuatia tukio hili kwa njia za mawasiliano ya kijamii. RealAudioMP3

Baba Mtakatifu anasema, Yesu Kristo, Mwana wa Mungu na Mkombozi wa ulimwengu amezaliwa mjini Bethlehemu kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kama utimilifu wa unabii wa kale. Ni mtoto wa Bikira Maria na mchumba wake ni Yosefu, watu wanyenyekevu, waliojazwa matumaini na wema wa Mungu, wanaompokea na kumtambua Yesu, kama ambavyo Roho Mtakatifu alivyowawesha wachungaji wa Bethlehemu waliotoka na kwenda kwa haraka kumshuhudia Mtoto Yesu. Ni Roho Mtakatifu aliyewaongoza akina Mzee Simeoni na Anna kwenye Hekalu la Yerusalemu na hapo wakamtambua Masiha na kuuona wokovu ambao Mwenyezi Mungu alikuwa amewaandalia watu wote.

Baba Mtakatifu anasema, Yesu Kristo ni wokovu wa kila mtu na kila taifa. Anamwomba ili aweze kuwaangalia Wakristo wanaoishi huko Iraq na Syria ambao kwa muda mrefu wanateseka kutokana na vita pamoja na watu wa makabila na dini nyingine wanaoendelea kudhulumiwa na kunyanyaswa. Noeli iwe ni chemchei ya matumaini kama ilivyo kwa wakimbizi na wahamiaji; watoto, na wazee kutoka sehemu mbali mbali za dunia; wanaongaliwa kwa “jicho la kengeza”; wanaokataliwa bila kuwasahau watu wenye shida na mahangaiko makubwa kutokana na baridi kwa wakati huu, ili waweze kurejea tena makwao ili kuishi kwa heshima na utu kama binadamu.

Baba Mtakatifu anamwomba Yesu Kristo, Mfalme wa amani, awajalie imani na amani watu wanaoishi Mashariki ya Kati, kwa kuanzia Nchi Takatifu mahali alipozaliwa, kwa kuenzi jitihada za wale wanaojikita katika majadiliano kati ya Waisraeli na Wapalestina. Baba Mtakatifu anamwomba Yesu Mkombozi awaangalie watu wanaoteseka huko Ucrain kutokana na vita na kinzani, ili washinde kishawishi cha chuki na vita, waanze hija ya udugu na mshikamano.

Baba Mtakatifu anaombea amani nchini Nigeria hata wakati huu bado kuna damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumwagika; kuna watu wametekwa nyara na wanaishi katika mazingira magumu au wameuwawa kikatiliki. Baba Mtakatifu anaendelea kuombea amani kwa nchi za Kiafrika kwa namna ya pekee: Libya, Sudan ya Kusini na DRC; anawasihi viongozi waliopewa dhamana ya kisiasa kujizatiti zaidi katika majadiliano, ili kushinda kinzani na hatimaye waweze kujenga na kuimarisha amani na udugu.

Baba Mtakatifu anamwomba Yesu Mkombozi awaokoe watoto wanaoteseka kwa mauaji, wanaogeuzwa kuwa kama bidhaa na kuuzwa katika soko haramu la binadamu, au wanalazimika kwenda mstari wa mbele kama chambo vitani. Yesu awe ni faraja kwa familia zinazoomboleza kwa kuondokewa na watoto wao waliouwawa kikatili nchini Pakistan hivi karibuni.

Yesu awe karibu na watu wanaoteseka kutokana na magonjwa, lakini kwa namna ya pekee ugonjwa wa Ebola, hasa nchini: Liberia, Sierra Leone na Guinea. Anawapongeza watu wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia watu walioathirika kwa ugonjwa wa Ebola, Baba Mtakatifu Francisko anaiomba Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, watu hawa wanapata huduma na tiba muafaka.

Mama Kanisa anapoadhimisha Siku kuu ya Noeli, kuna watu wengi wanaoendelea kulia na kuomboleza; machozi yao yanaungana na machozi ya Mtoto Yesu. Roho Mtakatifu awaangazie Watu wa Mataifa waweze kumtambua Mtoto Yesu aliyezaliwa Bethelehemu na Bikira Maria, zawadi ya wokovu iliyotolewa kwa watu wote duniani.

Nguvu ya Yesu Kristo inayojionesha katika kukomboa na kuhudumia, isikike tena mioyoni mwa watu wanaoteseka kutokana na vita, dhuluma na utumwa. Kwa nguvu ya upole wake wa Kimungu ang’oe mioyo migumu ya watu waliomezwa na malimwengu, kiasi hata cha kutoguswa na mahangaiko ya jirani zao. Nguvu yake inayokoa igeuze silaha kuwa majembe; uharibifu kuwa ugunduzi; chuki igeuke kuwa upendo na huruma, ili watu waweze kusema kwa furaha “Macho yetu yameuona wokovu wako”!

Baba Mtakatifu Francisko anawatakia watu wote Noeli Njema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.