2014-12-25 09:59:21

Iweni sababu ya furaha kwa wengine!


Katika mkesha wa Noeli, Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Masiha na Mkombozi wa ulimwengu, anayekuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti; kutoka katika giza na kumwonesha mwanga wa maisha na matumaini mapya. Utumwa kama ilivyokuwa kwa Waisraeli katika Agano la Kale, ni kielelezo cha mateso, mahangaiko na hali ya kukata tamaa.

Kumbe, kuzaliwa kwa Yesu Kristo kama ilivyotabiriwa na Manabii katika Agano la Kale ni ishara ya neema ya Mungu inayotaka kumfunda mwanadamu kutenda mema na kuachana na uovu pamoja na mabaya katika maisha. Kwa bahati mbaya, Kipindi cha Noeli kimevamiwa na kugeuzwa kuwa ni muda muafaka wa biashara, kiasi cha kupoteza maana halisi ya Noeli ambayo kimsingi inapata chimbuko lake katika mazingira ya kipagani, lakini, Kanisa likaitamadunisha na kuwa ni Siku ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mkombozi wa dunia!

Noeli inayoadhimishwa tarehe 25 Desemba ya kila mwaka, ikapata mwelekeo wa pakee katika Fumbo la Umwilisho, pale ambapo Neno wa Mungu alipotwaa mwili na kukaa kati ya binadamu na katika mambo yote alikuwa sawa na binadamu, isipokuwa hakutenda dhambi. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Kesha la Noeli, tarehe 24 Desemba 2014. Siku kuu hii bado inapata upinzani kutoka kwa wapinga Kristo ambao hata pamoja na kujiita kuwa ni "Wakristo bado imani yao inatia shaka: Fumbo la Umwilisho, Fumbo la Pasaka na Ekaristi takatifu".

Hawa ni watu ambao wanajizolea umaarufu mkubwa katika vyombo vya upashanaji habari kwa kuyakita mahubiri yao katika miujiza: kulisha, kuponya na utajiri. Askofu Niwemugizi anasema, tarehe si hoja, jambo linalopewa kipaumbele cha kwanza ni Fumbo la Umwilisho!

Siku ile alipozaliwa Yesu, Malaika waliwapasha watu habari juu ya tukio kuu katika historia ya maisha ya mwanadamu, wachungaji wakakimbia kwa haraka kwenda kustaajabia matendo makuu ya Mungu na Mamajusi kutoka Mashariki wakafunga safari kwenda kumwona na kumsujudia Masiha aliyezaliwa mjini Bethlehemu. Wachungaji walikuwa ni maskini watu waliokuwa wanakabiliwa na changamoto mbali mbali za maisha kama ilivyo kwa watu wa nyakati hizi.

Askofu Niwemugizi anasema, kuna watu wanateseka na kuhangaika: kiroho na kimwili; hawana matumaini ya kesho iliyo bora zaidi kutokana na magonjwa, ukosefu wa fursa za ajira, ukata, hofu, mashaka na wasiwasi. Kuna wafungwa na mahabusu gerezani ambao hawajui hatima ya maisha yao, lini kesi zao zitasikilizwa na haki kutendeka. Kuna waamini wana vifungo vya maisha ya kiroho kiasi kwamba, wanashindwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Wote hawa wanahitaji ukombozi na matumaini mapya yanayoletwa na Yesu Mkombozi wa ulimwengu!

Askofu Niwemugizi anasema, hali ya amani na usalama nchini Tanzania kwa mwaka 2013, ilikuwa inatisha kiasi cha kuwalazimisha waamini kusali mapema jioni, kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao, lakini kwa sasa mambo yamebadilika, waamini wameweza kwenda kusali na kushiriki kikamilifu katika kesha la Noeli kwa amani na utulivu, matendo makuu ya Mungu. Hizi zote ni changamoto zinazohitaji kukombolewa.

Kuna baadhi ya waamini hata katika Kipindi hiki cha Noeli, wanaendelea kushikwa na simanzi pamoja na huzuni kwa kuondokewa na wapendwa wao; kwa kukosa nafasi ya kukutana na kumujuika na ndugu na jamaa zao kutokana na sababu mbali mbali. Kuna watu ambao wanaandamwa na ukata, kiasi kwamba, hawana uhakika wa maisha yao wakati huu wa Kipindi cha Noeli. Kuna watoto ambao hawakubahatika kupata nguo mpya kwa ajili ya kusherehekea Noeli na Mwaka Mpya!

Askofu Severine Niwemugizi anawakumbushwa waamini wote hawa kwamba, jambo la msingi ni kutambua kwamba, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili anakuja kati yao, Yeye ni sababu ya furaha na matumaini yao; ni chemchemi ya upendo, furaha, amani, utulivu na matumaini. Wakati wa Majilio, waamini walihimizwa, kujenga moyo na utamaduni wa subira na matumaini, kwa kumsubiri Yesu Mkombozi wa dunia, ili aweze kuzaliwa tena katika maisha yao. Ujio wa Yesu, ambao kimsingi ni kielelezo cha imani, matumaini, mapendo, amani na mshikamano, uwapatie mwelekeo mpya wa maisha.

Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Yesu, mwanadamu amekombolewa kutoka katika lindi la dhambi na mauti; hiki ni kiini cha imani inayotangazwa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake. Yesu ni neema ya Mungu inayosafisha, takasa na kuokoa. Yesu ndiye Masiha, Mkombozi na Mpakwa wa Bwana wenye uwezo wa kifalme, kikuhani na kinabii mabegani mwake.

Askofu Niwemugizi anasema, Noeli ni kipindi cha kujisadaka, kujitoa na kujimega kwa ajili ya kuwashirikisha wengine ile furaha ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mkombozi wa dunia. Ni kipindi cha kujikana, ili jirani waweze kufaidika zaidi, kama ilivyokuwa kwa Yesu Kristo mwenyewe aliyeteseka, ili kumkirimia mwanadamu furaha, matumaini na maisha ya uzima wa milele. Yesu Kristo ndiyo sababu ya furaha ya kweli katika maisha ya mwanadamu.

Hii ni changamoto kwa waamini kukumbatia Injili ya Maisha na kuachana kabisa na tabia ya kufumbata utamaduni wa kifo unaosababisha machungu, simanzi na huzuni katika jamii. Hiki ni kishawishi kibaya kinachopaswa kuepukwa. Wakristo wanapaswa wasiwe ni sababu ya huzuni kwa jirani zao, kwa kujifunza kutokana na makosa, ili kutenda kwa kuwajibika zaidi. Uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika nchini Tanzania katika siku za hivi karibuni, hakwenda sawasawa, changamoto ya kujifunza kwa makosa kama haya, ili kufanya maboresho zaidi. Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli, iwe ni sababu ya furaha kwa wengine!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.All the contents on this site are copyrighted ©.