Hivi karibuni, katika maadhimisho ya Siku ya Haki Msingi za Binadamu Kimataifa, Ubalozi
wa Ufaransa nchini Benin, umewatunukia tuzo watawa wa Shirika la Wafranciskani wanaotekeleza
utume wao nchini Benin kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya
Uhai kwa kuokoa maisha ya watoto ambao hawajazaliwa, kwani hii ni haki yao msingi!
Ubalozi
wa Ufaransa unawapongeza na kuwataka watawa hawa kuendelea kutekeleza dhamana hii
nyeti bila kukata tamaa wala kuyumbishwa na walimwengu, kwani huu ni wajibu wao msingi.
Kwa miaka mingi, Watawa hawa wamekuwa mstari wa mbele kupinga mila na desturi zilizopitwa
na wakati, kwa kuwatoa watoto wadogo kama kafara, pale wanapozaliwa huku wakiwa na
kasoro katika miili yao. Kila mtoto ana haki ya kuzaliwa na kuishi kama watoto wengine
kwani hii ni haki yake msingi!
Umefika wakati kwa watu kuachana na mila na
tamaduni zilizopitwa na wakati kwa ajili ya kutafuta utajiri, madaraka na bahati katika
maisha! Maisha bora yanapatikana kwa kufanya kazi kwa juhudi, maarifa, nidhamu na
weledi na kwamba, hakuna njia ya mkato katika maisha!