2014-12-24 06:35:14

Papa asema: huduma ni kukidhi hitaji linalolengwa.


Jumatatu, 21 Desemba 2014, nyakati za adhuhuri, Baba Mtakatifu alikutana na wafanyakazi wa Vatican na Ofisi za Curia ya Roma, baada ya kukutana na Wakrugenzi na Maofisa wa ngazi za juu wa Jimbo Takatifu na utawala wa Vatican. Madhumuni ya Mkutano huu ilikuwa kutakiana heri za Siku Kuu ya Noeli.

Hotuba yake kwa wafanya kazi wote wa Vatican iliongozwa na maneno ya Mtakatifu Augustino aliyesema ni majivuno yaliyomfanya malaika kuwa ibilisi, na ni unyenyekevu unao wafanya watu kuwa sawa na malaika.

Baba Mtakatifu Francisco, pamoja na kutoa shukurani kwa idadi kubwa ya wafanyakazi wazawa wa Italia, pia kwa namna ya pekee aliwashukuru pia wafanyakazi kutoka mataifa ya nje ya Italia , ambao kwa ukarimu wamejitoa katika huduma ya Kanisa , mbali na nchi zao na familia zao , na hivyo kuwakilisha sura ya Kanisa moja la ulimwengu.

Kama ilivyokuwa katika hotuba yake kwa Wakuu wa Idara za Curia ya Roma ,pia kwa wafanyakazi wa kawaida, Papa alisisitiza umoja wa Kanisa kama ilivyo katika viungo vya mwili wa mtu , ni vingi lakini vyote hufanya kazi kwa kushirikiana , na hivyo unakuwa ni mfano mzuri hai kwa mwili wa Kristo ambalo ni Kanisa lake Takatifu. Kwa mtazamo huo Papa aliwaalika wote, kuchunguza dhamiri na kutafakari vyema wakati huu wa kipindi cha Noeli na mwaka mpya . Alihimiza kurejea katika sakramenti ya upatanisho kwa moyo mnyenyekevu , na kumpokea kwa upendo Bwana anayebisha hodi katika mlango wa roho , kumpokea kwa furaha ya familia.

Papa aliwashukuru wote akisema kila mmoja wao ana thamani kubwa katika utumishi wote, kama tu ulivyo mwili, kila kiungo, uwepo wake ni muhimu. Na wao ni viungo katika mwili wa Curia ya Roma .

Papa aliendelea kueleza kuwa huduma maana yake ni ufanikishaji wa lengo, ina maana kutazama kwa makini, mahitaji ya anayehudumiwa, ina maana ya kukubali kutoa au kupokea huduma. Papa aliwapa mfano wa mama anaye hudumia mtoto wake mgonjwa, mama huyo hujali katika hali zote maumivu ya mwanawe. Yeye kamwe hatazami saa , wala kulalamika kutokana na kutolala usiku wote, lakini anacho jali zaidi ni mtoto wake kuondokana na hali ya maumivu hayo kwa gharama yoyote.

Kwa maneno hayo, Papa aliwasihi kukifanya kipindi hiki cha Noeli kuwa wakati muafaka kwa ajili ya kuponya kila jeraha la uchungu wa uhaba wa huduma na kupajaza kila palipo pungukiwa.

Alisema, huu ni wakati wa kutibu maisha ya kiroho, na kujenga uhusiano wako na Mungu, kwa sababu huu ni uti wa mgongo, kwa kila jambo tunalolifanya na kwa kila jinsi tulivyo. Mkristo ambaye hajilishi kwa sala, sakramenti na Neno la Mungu, ni wazi hufifia na kunyauka na kufa. Kutibu maisha ya kiroho,
au kutibu maisha ya familia, kuwapa watoto na wapendwa wengine si fedha tu, lakini wakati wote, huduma na upendo.
Ni wakati wa kutibu mahusiano na watu wengine , kuleta upya wa imani katika maisha na maneno na matendo mema, hasa wale wanaohitaji zaidi. Ni wakati wa kutibu majadiliano, kusafisha lugha na maneno yenye kukera, kuondokana na lugha ya matusi na kihuni. Ni kupona majeraha ya moyo kwa mafuta ya msamaha, kuwasamehe wale waliotujeruhi kiroho na kuomba msamaha kwa majeraha tuliyo sababisha kwa wengine.

Ni wakati wa kuhudumu kwa moyo wenye shauku, unyenyekevu, ustadi, na hamu ya kujua jinsi ya kumshukuru Bwana, huu ni wakati wa kutafuta kutibu dhidi ya moyo wa wivu, tamaa, chuki na hisia hasi zenye kukumeza amani ya ndani na yenye kubadilisha watu kwa ndani na kuwa watu wa kuharibiwa na uharibifu, ni wakati wa kutibu uchungu wenye kuleta moyo wa kisasi, na uvivu ambayo unaongoza kwa katika hamu za kutaka msaada wa kuondosha maisha, kwa kuongozwa na kiburi, na malalamiko ya mara kwa mara yanayoongozwa na kukata tamaa.

Papa alieleza na kusema anazielewa hali hizi , ambazo hatima yake haiishii pazuri, bali katika uharibifu .Na hivyo amemwomba Bwana , hekima iweze kuuongoza ulimi wakati mazungumzo , si kusema maneno ya matusi, ambayo huacha uchungu kinywani.

Papa ameomba wote kutafuta huduma ambamo Roho wa Krismasi , isigeuzwe kuwa Siku kuu ya ulaji wa kibiashara , au utoaji wa zawadi zisizo kuwa na manufaa , lakini iwe ni sikukuu ya furaha ya kumjongea Bwana katika pango la Noeli lililomo ndani ya moyo.

Papa ameomba ili kwamba, Krismasi hii na iwe katika uhalisi wake wa kuwa Sikukuu ya umaskini wa Mungu ambaye alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa (cf. Phil 2,6); Mungu anayejiweka katika utumishi (Mat 22:27); Mungu aliyewaficha wenye hekima na akili, na kuwafunulia walio wadogo na maskini (Mat 11:25); "Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa maisha yake kuwa fidia ya wengi" (Marko 10:45).

Zaidi ya yote , hii ni sikukuu ya Amani inayoletwa duniani na mtoto Yesu, "Amani kati ya mbingu na nchi, amani miongoni mwa watu wote, amani katika mioyo yetu; amani kuimba pamoja na na malaika: "Utukufu kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema" (Lk 2:14). Amani kama hitaji katika shauku zetu, katika huduma zetu, na katika kutia joto katika moyo wenye baridi, yenye kuzihamasisha roho zilizopondeka kwa huzuni, amani yenye kuangaza wepesi wa macho wepesi, katika kuuona mwanga wa uso Yesu!
Kwa amani hii, Papa alikamilisha na maneno ya kuwatakia kila la heri wafanyakazi wote wa Vatican na familia zao, na pia aliomba msamaha kwa mapungufu yake mwenyewe binafsi na kwa niaba ya kanisa , kwa baadhi ya kashfa zinazo sababisha madhara kwa Kanisa. Aliwaomba pia wasisahau kumwombea.All the contents on this site are copyrighted ©.