2014-12-24 08:44:39

Ombeni hekima ya majadiliano, furaha na matumaini!


Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina, katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutambua kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu na kwamba, hii iwe ni changamoto kwao kutangaza na kudumisha amani ambayo kimsingi ni zawadi kubwa inayotolewa na Mwenyezi Mungu katika Siku kuu ya Noeli. RealAudioMP3

Ujumbe wa Malaika usikike tena mioyoni mwa watu “Amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema”. Maaskofu wa Argentina wanasema, Noeli ni kielelezo cha ukubali wa Mwenyezi Mungu kuendelea kumsindikiza mwanadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani, ili kujenga na kuimarisha ulimwengu ambamo haki, amani, upendo na mshikamano vinaweza kutawala tena katika mioyo ya watu.

Noeli ni kipindi cha kuimarisha umoja na udugu; msamaha na upendo; uhuru na kiasi, kwa wazazi kusameheana na watoto wao na watoto pia kuthubutu kuomba msamaha pale walipowakosea wazazi wao, tayari kuanza upya na kutembea katika mwanga wa Kristo, Mfalme wa Amani. Noeli ni siku kuu ya mshikamano na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Maaskofu wanawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha kwanza katika kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani mioyoni mwao, sehemu ambayo imeathirika kutokana na dhambi ya asili. Myumbo wa uchumi kimataifa inaendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya watu, kiasi kwamba, watu wanakumbatia utamaduni wa kifo kwa kutema Injili ya Uhai, haki msingi kwa kila binadamu.

Biashara haramu ya dawa za kulevya inaendelea kushamiri na kusababisha majanga kwa vijana na familia nyingi; bila kusahau biashara haramu ya binadamu; mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu; huu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Kumeibuka watu wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani wanaosababisha vifo, mateso na mahangaiko kwa watu wasiokuwa na hatia.

Lakini ikumbukwe kwamba, chuki na uhasama ni giza linalofunga mlango wa majadiliano na upatanisho kati ya watu. Rushwa na ufisadi wa mali ya umma ni majanga ya kitaifa yanayohitaji toba na wongofu wa ndani kwa kujikita katika uadilifu, ukweli na uwazi, bila kukumbatia uchu wa mali, ubinafsi na uchoyo. Waamini na watu wenye mapenzi mema, wajitahidi kujenga na kuimarisha mshikamano wa upendo na udugu, kwa kutafuta mafao ya wengi; utu na heshima ya binadamu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina linahitimisha ujumbe wake kwa Siku kuu ya Noeli kwa kuwataka waamini kumwomba Mwenyezi Mungu busara na hekima katika majadiliano; furaha na matumaini yasiyodanganya kamwe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.