Mpendwa mwanatafakari, unayeitegea sikio Radio Vatican, kwanza ninakutakieni heri
na baraka tele za kuzaliwa Mwana wa Mungu. Leo ni Noeli, ni neema ya Mungu iliyofunuliwa
kwetu.
Kwa hakika
ile ahadi ya Mungu aliyoitoa tangu zamani sasa imefunuliwa na hivi tunafurahi na kushangilia
tukiimba utukufu kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema. Mtoto
Emanueli aliye na uweza wa kifalme mabegani mwake, Mungu pamoja nasi amezaliwa kwa
ajili yetu. Kanisa duniani kote linaimba “pangoni Batlehemu amezaliwa mtoto Yesu,
twendeni sote tukamwone na kumpa zawadi”
Nabii Isaya anayeishi karne ya nane
kabla ya Kristu, anaonesha katika masomo ya sherehe za Noeli, jinsi Waisraeli wanavyofurahi
kurudi nyumbani toka utumwani Babeli. Wanafurahi kwa sababu wamekaa chini ya kandamizo
la utumwa kwa muda mrefu, na kandamizo hilo lilikuja kwa sababu wao wenyewe walishindwa
kutii mausia ya Mungu ,wakaingia katika ugomvi kati yao na hivi wakapelekwa utumwani.
Sasa Nabii Isaya akiona mwisho wa utumwa huo katika maono, anaimba akisema “watu wote
waliokwenda katika giza wameiona nuru kuu, na wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa
mauti, nuru imewaangaza”.
Uaguzi huu wa Nabii Isaya unakamilika kwa kuzaliwa
Masiha, Mwana wa Mungu, aliye mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele
na mfalme wa amani. Enzi yake haina mwisho, atahukumu kwa haki. Na kwa hakika hakuna
mfalme mwingine kabla na baada yake aliyeweza kuwa na sifa hizi.
Huyu aliyezaliwa
ni Neno wa Mungu, na ni Mungu mwenyewe ambaye ameshuka kutuambia alichotaka kutuambia
yaani upendo na kisha maisha ya uzima wa milele. (Mk. 9:7) Neno huyu asili yake ya
milele ni Umungu (Mk 1:1, Yn 1:1-2) na anapokuja kwetu ana asili ya pili yaani ubinadamu.
Ni Mungu mtu. Kuja kwake kulikuwa kwa lazima katika mantiki ya upendo usiopimika kwa
mwanadamu. Upendo huu ulitaka kufidia na kutoa sadaka timilifu mbele ya Mungu ukitaka
kufikia kile ambacho hakikuweza kufikiwa kwa ajili ya ubaya wa kumkataa Mungu uliotendwa
na wazazi wa kwanza.
Katika nyakati zetu nasi tuko utumwani, tuko katika taabu
mbalimbali kama vile ukosefu wa mahali pazuri pa kuishi, shida ya umeme, ukosefu wa
miundo mizuri kwa ajili ya matibabu, maji, sukari, rushwa na ugomvi kati yetu, upotevu
wa raslimali ya taifa pamoja na ajali barabarani. Je haya amesababisha nani? Ni sisi
wenyewe. Sasa leo Nuru imetushukia kutoka mbinguni kama tulivyokuwa tukiimba wakati
wa majilio “ushukie Masiha kuwakoa watumwao”.
Kushuka kwa Nuru ni kutaka kuondoa
giza ambalo ni kinyume na mwanga ambayo ndo hali ya Kimungu (kumbuka Mw. 1:2, mwanga
uwe na ukawa!). Mungu ndiye mwanga halisi wa vyote vilivyopata kuumbwa. Na hivi Mwana
wa Mungu aliye Neno wa milele anao uwezo na ndo uwezo wenyewe wa kufukuza giza na
kuwaangazia wengine (Yn 1:4-9). Je kuzaliwa kwa Bwana au kushuka kwa Nuru hii kwatufanya
kweli tuonje lile pendo la kweli walilolionja Waisraeli toka utumwani Babeli, kutoka
giza na kandamizo la shetani? Ewe mpendwa, Mwana wa Mungu ni Emanueli anakuja kutuondolea
utumwa, cha msingi tuaanze pamoja naye kuacha ubaya na kutenda wema.
Tutafakari
vema wajibu wetu, katika kuondoa matatizo yaliyoainishwa, tuwe makini katika upigaji
wa kura ili kuwapata viongozi watakaotunza mali zetu. Tujitahidi wewe nami kutokuwa
sehemu ya mlango pitishi wa mali hizo. Kwa namna hii wimbo wa ushukie Masiha utakuwa
wa kweli na furaha ya ujio wa Masiha itakuwa ya kweli.
Kuacha ubaya na kutenda
wema ni ujumbe kamambe ambao Mtume Paulo anamtumia Mtakatifu Tito akimsistizia kuwa
Neema ya Mungu Mwokozi, inayookoa wanadamu wote imefunuliwa kwetu na hivi kazi yetu
kama twataka kuifaidi neema hiyo ni kuambatana na maisha ya uongofu, maisha ya kupokea
na kuzitumia neema za Mungu pamoja nasi, yaani Emanueli. Kuzaliwa kwa Kristu ni amani
na uhuru kwa wana wa Mungu, ni ufunuo mkamilifu wa Mungu, kwa maana tangu zamani Mungu
alisema nasi kwa njia ya Mababu, Manabii na sasa anasema nasi kwa njia ya Masiha,
Mwanae mpenzi tunaye paswa kumfuata.
Mpendwa mwana Noeli, Mwinjili Luka akitupeni
habari ya furaha, kwanza anamweka Bwana katika mazingira ya mwanadamu. Anaweka mbele
yetu kwanza jambo la kijiografia na la kihistoria, akisimulia juu ya Masiha anayezaliwa
wakati wa mfalme wa Kirumi Kaisari Augusto, pia anazaliwa Betlehem kijiji cha wachungaji
kama ilivyokuwa imeaguliwa kwamba atazaliwa katika ukoo wa Daudi. Hili laonesha kuwa
Masiha anaingia katika maisha ya mwandamu.
Pamoja na hilo pale pangoni Betlehemu
anashuhudiwa na wachungaji kielelezo cha upendo wa Mungu kwa wote na hasa walio fukara
na maskini, na kwa jinsi hiyo Mungu atufundisha kushinda uovu si kwa vita bali kwa
upendo na msamaha.
Wote twatambua kuwa wachungaji wakati ule walikuwa ni watu
wa kulala machungani, waliodharauliwa na hata hawakuruhusiwa kuingia kwenye masinagogi,
walikuwa wakisadikika kuwa waongo na wagomvi. Mwana wa Mungu anaona hao ndio wapewe
habari ya kuzaliwa kwake wakiwa wa kwanza. Maana yake Mungu ni kwa ajili yao na anachagua
kukaa katikati yao, yaani walio maskini. Mwinjili Yohane anaweka mbele ya mataifa
Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili na akakaa kwetu. Masiha ni Neno wa Mungu ambaye anatumwa
na Mungu kwetu kwa sababu ya upendo upeo. Ni nuru ileile ambayo Nabii Isaya anaitangaza
katika Agano la kale ya kwamba miisho yote ya dunia imeiona nuru na wokovu wa Mungu.
Mungu
amefanyika mwili nasi tukauona wokovu wake na hivi tunaalikwa kusikiliza na kutenda
kadiri ya mapenzi yake. Mwinjili Yohane anatupatia Fumbo la Umwilisho kielelezo wazi
cha upendo wa Mungu, Mungu anayejishusha na kutwaa mwili wako dhaifu! Anataka kugeuza
mwili wako uwe mwili wa utukufu. Kwa fumbo hili la Bwana kukaa kwetu, ni fundisho
la amani kwa mataifa, kumbe kugombana tishio dhidi ya upendo uliowekwa kwa njia ya
fumbo la umwilisho katika jamii ni kinyume na fumbo la Noeli.
Yafaa basi,
kufikiri kidogo juu ya vita vinavyoendelea duniani, juu ya madhulumu katika nchi yetu
kiasi kwamba umeingia wasiwasi mkubwa kinyume na utlivu tulikuwa nao mwanzoni. Kumbe
Neno akafanyika mwili ni nuru na amani kwa watu wote. Ni sura na utukufu wa Mungu
Baba na kielelezo cha mapendo yasiyopimika kwa Mwanadamu, na kwa namna hiyo kila mmoja
wetu afikiri sana juu ya mchango wake katika kujenga amani au kuibomoa!
Ninakukumbusha
kuwa Bwana amekuja na kukaa kwetu, maana yake anakaa kwenye familia, kumbe ni sherehe
ya familia ni siku za kukaa pamoja Baba mama na watoto. Na kama vile ambavyo mtoto
anapozaliwa tunapeleka habari ya furaha kwa majirani basi kukaa kwetu pamoja na Bwana
katika familia kuwe ni chimbuko la habari njema ya furaha kama Wachungaji walivyopeleka
habari njema ya furaha kwa watu wote.
Kumbuka kule Betlehemu Bwana alikosa
nafasi katika nyumba ya wageni na hivi asije akakosa nafasi katika moyo wako katika
sherehe hizi za Noel na daima. Nafasi ya Bwana yapaswa kutayarishwa daima kwa maisha
ya sala na sakramenti. Kuna desturi ya kubatiza watoto katika sikukuu ya Noeli, yafaa
kuelewa kuwa ni nafasi muhimu na ya pekee inayotayarisha mahali Bwana atakapokaa katika
mtoto huyo, kumbe wazazi itunzeni nafasi iletwayo kwetu kwa njia ya ubatizo kwa njia
ya zawadi hii kubwa inayotufanya kuwa watoto wa Mungu na Kanisa.
Ninakutakieni
heri na baraka tele za Mungu, Noeli njema. Tumsifu Yesu Kristo, Maria na Yosefu.
Tafakari
hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya, C.PP.S.