Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Yohana Sefue, amemsimamisha kazi kwa muda Ndugu
Eliakim Maswi, Katibu Mkuu ya Wizara ya Nishati na Madini, ili kupisha uchunguzi wa
tuhuma dhidi yake, kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Balozi Sefue amemsimamisha kazi Ndugu Maswi
kuanzia, Jumanne, Desemba 23, 2014, kwa kutumia madaraka aliyonayo kama Mamlaka ya
Nidhamu kwa Watumishi wa Umma wanaoteuliwa na Rais, wakiwemo Makatibu Wakuu. Taarifa
iliyotolewa na Ofisi ya Balozi Sefue mjini Dar es Salaam imesema kuwa amechukua hatua
hiyo “Kwa mujibu wa Kifungu 4(3) (d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Na. 8 ya mwaka
2002 (kama ilivyorekebishwa)” ambapo “Katibu Mkuu Kiongozi ndiye Mamlaka ya Nidhamu
kwa Watumishi wa Umma wanaoteuliwa na Rais, wakiwemo Makatibu Wakuu.”
Badala
yake, Balozi Sefue amesema kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi
Ngosi C. Mwihava atakaimu nafasi ya Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, hadi
uchunguzi dhidi ya Ndugu Eliakim C. Maswi utakapokamilika.
Taarifa hiyo ya
Balozi Sefue pia imekariri kauli ya Rais Kikwete katika hotuba yake kwa Taifa jana,
Jumatatu, Desemba 22, 2014 ambako Rais alisema: “Kuhusu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini, kwa vile ni Mtumishi wa Umma, anatawaliwa na Sheria na Kanuni za
Utumishi wa Umma, hivyo nimeshaelekeza Mamlaka kuchunguza tuhuma zake na hatimaye
ikibainika ana makosa hatua za kinidhamu zitachukuliwa.”
Ndugu Maswi, aliyekuwa
Mwanasheria Mkuu Ndugu Frederick Werema pamoja na Mawaziri wawili walituhumiwa wakati
wa Kikao cha Bunge kilichopita kuhusiana na Akaunti ya Tegeta Escrow.
Wakati
huo huo, Rais Kikwete ameelekeza kuwa pamoja na hatua nyingine zinazochukuliwa, Shirika
la Umeme (TANESCO) waendelee na majadiliano na IPTL kuhusu uwezekano wa kushusha tozo
la uwekezaji (capacity charge) zaidi ya punguzo la awali lililopatikana kupitia Kituo
cha Kimataifa cha Kusuluhisha Migogoro ya Kimataifa (ICSID).