2014-12-24 09:17:13

Jengeni mshikamano wa upendo, ili kuwatangazia watu Injili ya Furaha!


Kadiri ya Mapokeo na mila njema kutoka Barani Afrika, Mtoto anapozaliwa inakuwa ni chemchemi ya furaha na matumaini kwa jamii inayomzunguka, changamoto na mwaliko kwa wanajamii kumtembelea na kumpatia zawadi, kama kielelezo cha matumaini. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Yesu, Mwana wa Mungu amezaliwa kati ya watu, ili kuonesha zawadi ambayo Mwenyezi Mungu amependa kumzawadia mwanadamu, kama chombo cha maisha yenye uzima mpya; amani, haki na upatanisho.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Padre Paul Samasumo, Mkuu wa Idhaa ya Kiingereza na Kiswahili ya Radio Vatican wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu katika Kikanisa cha Radio Vatican, Jumanne, tarehe 23 Desemba 2014, wafanyakazi na viongozi wakuu wa Radio Vatican, walipokusanyika kwa ajili ya kutakiana kheri na baraka katika maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli na Mwaka Mpya 2015.

Padre Samasumo anasema, Noeli iwe ni fursa kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, kusimama kidogo, ili kufanya tafakari ya kina pamoja na kumwachia Mungu nafasi ya kuweza kuzungumza na kila mmoja wao, kutoka katika undani wa maisha. Katika ukimya na tafakari, hapo mwamini anaweza kutibu madonda makubwa yanayomwandama katika maisha na utume wake. Waamini wajitahidi kumwachia Mwenyezi Mungu nafasi katika kufanya maamuzi makubwa ya maisha.

Katika Ibada hii ya Misa, Wafanyakazi wa Radio Vatican wamesali kwa ajili ya kuliombea Kanisa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake.

Padre Federico Lombardi, Mkurugenzi mkuu wa Radio Vatican akizungumza na wafanyakazi wa Radio Vatican, amewapongeza wafanyakazi ambao wamemaliza muda wa huduma Radioni; amewaombea wale wote waliopumzika katika usingizi wa amani pamoja na kuwapongeza wafanyakazi ambao wamebahatika kufunga ndoa na kupata watoto katika kipindi cha mwaka wa 2014.

Ni mwaka ambao umekuwa na magumu pamoja na changamoto zake, lakini pia ni mwaka ambao umeonesha cheche za matumaini kwa Serikali ya Cuba na Marekani kuanzisha mahusiano ya kidiplomasia baada ya nchi hizi mbili kuoneshana ubabe kwa zaidi ya miaka 53. Hizi ni jitihada za Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, kiongozi anayependa kujenga madaraja yanayowaunganisha watu!

Hii ni hija ya matumaini kama alivyoonesha Ibrahamu Baba wa Imani alipoambiwa na Mwenyezi Mungu kutoka katika nchi yake na kwenda kuanza maisha mapya ugenini. Radio Vatican inaendelea kushirikiana na Baba Mtakatifu Francisko katika kuwatangazia Watu wa Mataifa, Injili ya Furaha na Matumaini.Baba Mtakatifu Francisko ni kiongozi aliyekuja na mikakati, changamoto na vipaji ambavyo anavitumia katika kuliongoza Kanisa la Kristo!

Padre Lombardi anakiri kwamba, si haba, kwa hakika wafanyakazi wa Radio Vatican wamejitahidi kutekeleza wajibu wao ili kumsaidia Baba Mtakatifu kuwafikia watu wengi zaidi duniani. Kanisa, kama alivyokazia Baba Mtakatifu wakati akizungumza na wasaidizi wake wa karibu linahitaji kutibu madonda, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano; kwa kuzingatia upendo, utu na heshima ya binadamu; watu wajitajidi kufahamiana na kuchukuliana kwa saburi.

Padre Lombardi anaonya kwamba, chuki, kinzani na utengano kati ya watu kama haukupatiwa tiba na kwa wakati muafaka unaweza kuwa ni chanzo cha majanga. Wafanyakazi wa Radio Vatican wajitahidi kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano kati yao; mambo msingi yatakayowasaidia kutekeleza majukumu yao kwa furaha na majitoleo zaidi.

Kwa mwaka huu, kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya Radio Vatican, Ibada ya Misa Takatifu katika mkesha wa Noeli, inarushwa moja kwa moja kutoka Vatican kwenda Indonesia, ili kuwatangazia watu hao, Injili ya Furaha wakati huu wa Kipindi cha Noeli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.