2014-12-23 07:06:37

Ujumbe wa Noeli kutoka Yerusalemu!


Patriaki Fouad Twal wa Yerusalemu katika ujumbe wake kwa Siku kuu ya Noeli kwa mwaka 2014, anakumbuka kwa namna ya pekee, hija ya Baba Mtakatifu Francisko katika Nchi Takatifu na dhamana ya Kanisa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene; haki na amani kati ya watu kwa kuwakutanisha Marais wa Palestina na Israeli pamoja na viongozi wakuu wa dini mbali mbali mjini Vatican, ili kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani. RealAudioMP3

Anamshukuru Mungu kwa zawadi ya miito ya Upadre, inayoliwezesha Kanisa kuendelea kutoa huduma kwa Familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Maadhimisho ya Sinodi maalum ya Familia yaliyofanyika mjini Vatican mwezi Oktoba 2014, imekuwa ni nafasi kwa Mama Kanisa kusali, kutafakari na kushirikishana, fursa, matatizo na changamoto zinazoikumba familia katika ulimwengu mamboleo.

Kanisa linataka ili kweli kuendelea kutangaza Injili ya Familia kwa kukazia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, zinazojikita katika uaminifu, udumifu pamoja na kushiriki kikamilifu katika kazi ya uumbaji na malezi kwa watoto ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Familia katika Nchi Takatifu zinakabiliana na changamoto na matatizo makubwa, kwa baadhi ya wanandoa kukosa nyaraka muhimu zinazowawezesha kuishi kwa pamoja kama Bwana na Bibi katika maisha ya ndoa na familia. Baadhi ya familia zimetengana na kwamba, hivi karibuni baadhi ya familia hizi zimeunganishwa tena, jambo la kumshukuru Mungu.

Kanisa linatarajia kuwatangaza Mwenyeheri Maria Bawardi na Marie Alphonsine Ghattas kutoka Palestina kuwa watakatifu, tukio ambalo linatarajiwa kuhudhuriwa na umati mkubwa wa Familia ya Mungu kutoka Yerusalemu, kwani watakatifu hawa ni cheche za imani, matumaini na mapendo; wao ni waombezi wakuu kwa ajili ya kudumisha mchakato wa haki na amani huko Mashariki ya Kati.

Patriaki Twal anasema, mwaka huu umegubikwa pia na majonzi makubwa kutokana na vita na kinzani zilizopelekea maelfu ya watu wasiokuwa na hatia kupoteza maisha yao, wengine kupata ulemavu wa kudumu pamoja na kulazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na uharibifu mkubwa wa makazi ya watu. Wanasiasa wa Israeli na Palestina wasaidiwe na Jumuiya ya Kimataifa ili kupata suluhu ya kudumu, kuhusu mgogoro wa Israeli na Palestina.

Mauaji ya watu wasiokuwa na hatia ni changamoto kubwa katika kulinda na kudumisha haki na amani katika Nchi Takatifu; watu bado wanaendelea kumwaga damu huku wakitokwa na machozi ya uchungu; changamoto ya kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini, kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi.

Wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria na Iraq bado ni changomoto kubwa huko Mashariki ya Kati. Ni watu ambao wanateseka na kwamba, wanaishi katika mazingira magumu yanayohitaji mshikamano wa dhati kutoka ndani na nje ya Mashariki ya Kati. Inasikitisha kuona kwamba, kuna vijana wanapata ujasiri wa kujitosa kushiriki katika vita huko Mashariki ya Kati, ili kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia, dalili za vijana waliokata tamaa ya maisha, kiasi cha kukumbatia misimamo mikali ya kiimani.

Patriaki Fouad Twal anasema, kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mwana wa Mungu ni utimilifu wa upendo, huruma na amani kwa watu wanaoishi katika mazingira hatarishi; watu ambao maisha yao yananyakuliwa hivi hivi na kifo pasi na msaada kutokana na chuki za kidini. Patriaki Twal pamoja na yote haya anapenda kuwatakia waamini na watu wote wenye mapenzi mema, heri na baraka kwa Siku kuu ya Noeli na Mwaka Mpya 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.