2014-12-23 10:47:17

Ni Siku kuu ya "Akina yakhe pangu pakavu, tia mchuzi"!


Kila taifa hapa duniani lina zoezi la kuhesabu raia wake. Zoezi hilo linaloitwa Sensa. Lengo la senza ni kutaka kujua idadi ya wananchi. Enzi za utawala wa kifalme, kuhesabu watu lilikusudia kujua idadi ya raia walio chini ya himaya ya mfalme, hasa wale wanaoweza kulipa kodi ili mfalme aweze kupanga mikakati ya kuwahudumia ipasavyo.

Katika Biblia, zoezi la kuhesabu watu (sensa) lilichukuliwa kuwa ni majivuno. Hivi Mungu aliweza kumwadhibu, wafalme wa Israeli wanaohesabu watu. Kwa hoja kwamba haki ya kujua idadi ya watu ni ya Mungu peke yake aliyetuumba. Kwa hiyo utamaduni huo wa kutohesabu watu ni wa watu wote wa mashariki.

Leo tunakutana na utamaduni wa Magharibi (warumi) wa kuhesabu watu. Aidha, tutaona itifaki ya watu wakubwa ilivyojipanga. Kulitokea tangazo toka Mfalme Augusto Oktaviano. Mfalme huyu alizaliwa tarehe 23 Septemba. Kutokana na umaarufu wake aliouonesha, tarehe hiyo aliyozaliwa ikaja kuweka na kuwa mwanzo wa mwaka. Yaani mwanzo wa mwaka mpya kwa dola nzima. Bahati mbaya badaye mfalme huyo akafa na akaibuka Kaisari mwingine aitwaye Tiberius wa Livio, ndiye ambaye Yesu alikulia kipindi chake.

Tunaambia kuwa hiyo ilikuwa ni senza ya kwanza ambapo Kwirinio aliyekuwa Jemedari alipokuwa mkuu wa mkoa mkubwa kule Siria mji wake mkubwa ukiwa ni Antiokia. Kaisari Augusto Oktaviano alimjali sana huyo Kwirinio. Hivi mtu wa kwanza kuorodheshwa katika mchakato huu wa senza ni Kaisari Augusto ndiye anayehesabu watu, na mtu wa pili kwa umaarufu ndiye huyo Kwirinio.

Kama wakati wa senza hiyo alizaliwa Mungu basi huyo naye aliingia moja kwa moja katika orodha ya kuhesabiwa. Yeye ambaye ni mfalme wa wafalme, anayetakiwa kuhesabu watu wake na kujua idadi yao, sasa yeye mwenyewe anaingia kuhesabiwa. Amechukua umbo la mtumwa, kuonesha kwamba yeye toka milele ni mtumishi. Anaonesha mfano wa upendo unaobidi kuoneshwa na wakuu wa duniania hapa kwa raia wao.

Baada ya kuipitia orodha ya wakuu kama akina Kaisari Augusto Oktaviano na Kwirinio aliyekuwa anatawala mashariki yote sasa inaingia na orodha nyingine. Kwanza anatajwa Yosefu mseremala, wa ukoo wa Daudi, anafika Yerusalemu akitokea kijiji cha Nazareti cha huko Galilea. Baada ya jina la Yosefu anatajwa mke wake Maria akiwa mja mzito, wote wanafika kuhesabiwa. Halafu mwishoni ndo linatajwa jina la mtoto Yesu atakayezaliwa.

Itifaki hii ndiyo inayofuatwa na kuheshimiwa hapa duniani. Katika orodha hii ya watu wakubwa, Yesu anashika mkia. kinyume cha mategemo ya itifaki zinavyopangwa na kufuatwa hapa ulimwenguni. Kumbe mbinguni kunafuatwa utaratibu mwingine kabisa wa itifaki. Kwanza ni Mungu mwenyewe, halafu mama yake anayejiita “mtumishi wa Bwana”, halafu Yosefu anayeitwa “mwenye haki.”

Walipokuwa pale Betlehemu Maria alimzaa mtoto wake wa kwanza wa kiume. Baada ya kuzaa kunafuata mlolongo wa matukio pale pangoni yaani tunaletewa pahala alipozaliwa mtoto kisha kuna wachungaji na majusi. Halafu Maria anamviriga mtoto katika kitambaa. Hapa unaona jinsi mwinjili anavyonukuu Agano la kale.

Kule kuviringa mtoto katika kitambaa kunaleta wazo kwenye kitabu cha Hekima, wakati anazaliwa Salomoni “Anasema Salomoni, hata mimi ni mtu dhaifu, ….kama wengine sauti yangu ya kwanza ni kulia” Hakuna mfalme anaweza kuingia duniani kwa namna ya pekee. (Hekima …) Hivi huyu mfalme Yesu Kristu naye anaingia hivyo hivyo, analia na mama yake anamkumbatia. Mungu wetu amejionesha kama mtoto, asiyeweza kufanya kitu, ni Mungu anayehitaji kukumbatiwa, kubebwa, kumshangaa, kumstaajabia. Ni mtu kama sisi na kwa kujifanya mtu aliweza baadaye kufa.

Kisha akawekwa kwenye hori la kulishia wanyama. Hapa nyumba za kulala haimaanishi nyumba ya wageni. Kadiri ya ujenzi wa nyumba za kushi za wakati huo pembeni kulikuwa na sehemu ya kulala wanyama, na sehemu ya kulala watoto. Akina mama baada ya kuzaa, walimpeleka mtoto kukaa na mama sehemu ya pekee, ambako walikuwa wanakaa wanyama, ili kupata hewa na joto, mfano Nabii Isaya (wanyamma wamemtambua bwana wao lakini Waisraeli hapana). Kwa hiyo yaonekana mwinjili alikuwa na maana yake anaposema kuwa hapakuwa na pahala pa kulala, na kwamba mtoto aliwekwa horini, lakini hawakufukuzwa, kwa sababu watu wale walijali sana kupokea wageni, kwao ilikuwa ni jambo takatifu kupokea wageni.

Ila tatizo ni kwamba hapakuwa na nafasi. Lakini lengo la mwinjili ni kwamba alizaliwa huko kwa ajili ya kusisitiza ufukara wa Kristo. Ieleweke pia kwamba wakati Yesu anazaliwa ulikuwa ni wa Augusto Oktaviano yaani wakati watu walikuwa na maisha mazuri. Lakini Mfalme huyu anachagua kuzaliwa sehemu ya kifukara kama hiyo.

Kisha wanatamkwa wachungaji, na yaonekana ilikuwa ni kati ya miezi ya Machi hadi Oktoba, kwani kuanzia mwezi Novemba hadi Februari ni kipindi cha baridi. Wachungaji walidharaulika sana, hawakuwa kitu. Walikuwawanaishi milimani, walikuwa na maisha kama ya wanyama, ni watu waonevu, wenye wivu, hawakuweza kuruhusiwa kuingia hekaluni.

Malaika wa Bwana anawatokea hao. Wakahofu na kushangaa sana, kuonesha kwamba kwao hayo yalikuwa ni maono ya pekee waliyoyategemea. Wanaona mwanga wa pekee, yaani wanaona utukufu wa Mungu unaonekana kwao siyo kama ule wa kawaida. Mungu siyo kama mlivyofundishwa, Mungu wa kutisha, tena siyo kama Mungu anayekuja kuwakomboa wale walio hekaluni, wakuu, la hasha bali ni Mungu wa watu wanyonge. Ndivyo walivyoambiwa hata Zakayo, na mnyang’anyi wa Msalabani. Mwanga huu unakaa na wanyonge. “Kwenu leo …”.

Alama ya watakayogundua ya ukombozi ni mtoto, yaani siyo mtu mkubwa wa kutisha anayefika kuwakomboa, bali ni mtoto mdogo tu wa kawaida kama watoto wengine. Kinyume cha alama, vigezo vya thamani za vitu vinavyoweza kuwakomboa. Siyo mfalme Kaisari Augusto Oktaviani, anayekuja kuleta amani na haki, aliyeanzisha mwaka mpya Septemba, la hasha, bali habari njema inaanza pale Maria anapozaa mtoto, ndipo mwanzo wa mwaka. Yaonekana hata wakunga waliokuja kusaidia kuzalisha hawakuelewa kinachoendelea usiku ule, kwani alionekana kuwa ni mtoto wa kawaida tu. Lakini kumb huyu alikuwa wa pekee. Kweli pakawa mwanzo wa kuhesabu miaka. Hatimaye kuna utukufu unaoimbwa na kwaya ya malaika wanaimba “Utukufu kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema”.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.