Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 24 Desemba, 2014, anatarajiwa kuadhimisha
Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mkesha wa Siku kuu ya Noeli, katika Kanisa kuu
la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 3: 30 Usiku kwa saa za Ulaya. Ibada hii
ya Misa Takatifu itatanguliwa na wimbo wa Kalenda unaotangaza Fumbo la kuzaliwa kwa
Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, aliyetabiriwa na Manabii tangu Agano la Kale.
Yesu
Kristo ni kielelezo cha Agano Jipya kati ya Mungu na mwanadamu, ili aweze kumkirimia
tena amani na ustawi baada ya Waisraeli kutembea katika giza la maisha, katika utumwa
na mahangaiko mbali mbali utumwani Misri, hatimaye wakakombolewa kwa mkono wenye nguvu
kutoka kwa Mwenyezi Mungu, aliyekuwa anaambatana na Mtumishi wake mwaminifu Musa.
Kuzaliwa
kwa Yesu Kristo Mkombozi wa dunia ni tukio ambalo linafumbatwa katika historia ya
utawala wa Kirumi, uliokuwa chini ya Kaisari Oktaviani Augusto, wakati huo, amani
ilikuwa inatawala katika uso wa dunia, Yesu Kristo, Mwana wa Baba wa Milele, aliyetungwa
kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria, akawa Mwanadamu na kuzaliwa mjini
Bethlehemu. Kalenda ni wimbo wa sifa na utukufu kwa Yesu Kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika
mwili!
Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Siku kuu ya Noeli, majira ya saa
6: 00 Mchana kwa Saa za Ulaya, anatarajiwa kutoa ujumbe wake wa Noeli kwa mji wa Roma
na Dunia kwa ujumla na baadaye kutoa baraka yake ya kitume kama inavyojulikana kwa
lugha ya Kilatini "Urbi et Orbi". Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, itakuwa nawe
bega kwa bega ili kukujuza yale yanayoendelea ndani na nje ya Vatican, wakati huu
Mama Kanisa anaposherehekea Siku kuu ya Noeli.