2014-12-22 12:19:00

Ugonjwa wa Ebola bado ni tishio kwa maisha na maendeleo ya watu!


Ugonjwa wa Ebola ni kati ya majanga ambayo yametishia usalama na maisha ya watu wengi Afrika Maghariki katika kipindi cha Mwaka 2014 kiasi cha madaktari waliojisadaka maisha yao kupambana na ugonjwa huu kutajwa na Jarida la TIMES kuwa ni kati ya watu mashuhuri kwa Mwaka 2014. Wanachama wa Baraza la Makanisa Ulimwengu wamekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola huko Afrika Magharibi, kiasi cha kuunda kikosi kazi cha kufuatilia mapambano haya katika ngazi ya kimataifa.

Viongozi wakuu wa Makanisa wanasema kwamba, ugonjwa wa Ebola umeacha madhara makubwa sana katika maisha ya watu, kiasi hata cha kukwamisha mchakato wa maendeleo endelevu, mahusiano na mfungamano wa watu kimataifa. Baraza la Makanisa Ulimwenguni limeendelea kushirikiana na wadau mbali mbali ili kutoa huduma ya afya kwa wananchi wanaoishi vijijini katika zile nchi ambazo zimeathirika vibaya kwa ugonjwa wa Ebola.

Ili kufanikisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na wadau mbali mbali kutambua na kuthamini mila na desturi za Kiafrika kuhusiana na zawadi ya uhai, ili kuwasaidia wananchi waliokumbwa na ugonjwa huu kuweza kufuata protokali zinazotakiwa katika kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Ebola, vinginevyo, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kujikuta kwamba, mikakati na malengo yake hayafanikiwa kwa kama ilivyopangwa.

Umoja wa Mataifa umedhamiria kufanya kazi kwa kushirikiana na Makanisa Ulimwenguni, ili kutokomeza ugonjwa wa Ebola ambao bado ni tishio kubwa kwa maisha na maendeleo ya watu!All the contents on this site are copyrighted ©.