2014-12-22 09:21:05

Noeli ni kipindi cha imani, matumaini na mapendo!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kwa kitambo kidogo, ili kufanya tafakari ya kina maana ya Siku kuu ya Noeli katika mwono wake sahihi wa maisha ya kiroho na wala si kufunikwa na kampeni za biashara kama inavyojionesha kwa wakati huu. RealAudioMP3

Noeli inapambwa kwa maneno makuu yafuatayo: familia, zawadi, chakula na gharama zake. Ni kundi dogo sana la waamini nchini Ufaransa linalohusisha maisha ya kiroho na maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli.

Kardinali Andrè Vingt Trois, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Paris, Ufaransa anasema kwamba, Noeli inapaswa kuwa ni tukio linalowaalika waamini kuwashirikisha wengine ile furaha, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho; kwa kushuhudia mbele ya watu imani yao kwa Yesu Kristo Mwana wa Mungu. Kanisa nchini Ufaransa linataka kuwasaidia waamini kuhakikisha kwamba, kweli wanaadhimisha Fumbo la Umwilisho wakiwa na imani thabiti inayowaonjesha faraja na matumaini katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani.

Watu watambue kwamba, licha ya magumu na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha yao, Mwenyezi Mungu bado anaendelea kuwajali na kuwapatia tunza yake ya kibaba, kamwe hajawaacha kutembea katika utupu wao kwa kujikatia tamaa! Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanahamasishwa na Mama Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili na manyofu kuwa kweli ni vyombo vya Uinjilishaji na wajumbe wa haki, amani na matumaini kati ya watu.

Baraza la Maaskofu kwa kutumia mitandao mbali mbali ya kijamii linapenda kuwasaidia waamini kutambua maana halisi ya Kipindi cha Noeli katika maisha na utume wa Kanisa, bila kulazimisha watu, bali kufanya yote kwa sifa na utukufu wa Mungu. Kipindi cha Majilio, umekuwa ni wakati muafaka kwa Mama Kanisa kuinjilisha kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji, inayosaidiwa na mitandao ya kijamii.

Waamini wanaulizwa maswali ya msingi kuhusu Yesu Kristo, ili kuwachangamotisha kwenda pembezoni mwa Jamii ili kutafuta mambo msingi ya maisha, hasa katika kipindi hiki cha Majilio, ili kuwaonjesha wengine: furaha, imani, matumaini na mapendo. Mitandao ya kijamii, ikiwa kama inatumika barabara , inaweza kuwa ni chombo makini cha Uinjilishaji miongoni mwa vijana, kwani vijana hawa wanatumia muda wao mwingi wakiwa wanaogelea kwenye mitandao yao.

Huu ni utekelezaji wa changamoto inayotolewa na Mama Kanisa ya kuwasaidia vijana kupata majiundo makini yatakayowawezesha kuwa ni watumiaji wazuri ya mitandao ya kijamii kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.