2014-12-22 11:26:38

Mwanga wa Injili uendelee kuwaangazia Watu wa Mataifa katika mapito yao!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika ujumbe wake kwa Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2014 linawatakia Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema neema na baraka kwao wote, lakini zaidi kwa wale ambao wanalazimika kuyaacha makazi yao, kiwe ni kipindi cha kuangalia makusudi na upendo wa Mungu katika maisha yao, Mungu anayekuja kuwaletea mwanga wa imani na matumaini, ili waweze tena kutembea katika mwanga wake.

Dr. Olav Fyske Tveit anasema, katika ujumbe huu wa Noeli kwamba, Yesu Kristo ni Mfalme, aliyezima kiu ya Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali waliongozwa na nyota, ili kwenda kumtazama na kumsujudia Yeye aliyekuwa amezaliwa mjini Yerusalem. Kwa bahati mbaya, Mfalme Herode alishikwa na wivu hata kabla ya kumwona Mtoto Yesu! Wakati mwingine si rahisi kuweza kuona mwanga katika maisha, lakini jambo la msingi ni kuendelea kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukata tamaa.

Mamajusi walipokwisha kumwona Mtoto Yesu na kumsujudia walirudi makwao kwa kupitia njia nyingine, ili kuendelea kumwabudu na kumtukuza Mwenyezi Mungu; kuendelea kutangaza haki, amani, upendo na mshikamano, kwani hii ndiyo zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu anapenda kuwakirimia wanadamu katika kipindi hiki cha Noeli, kinachojumuisha pia Siku kuu ya Tokeo la Bwana, anapojifunua kwa Mataifa hadi pale anapobatizwa Mtoni Yordani, tayari kuanza maisha yake ya hadhara.

Mama Kanisa anaendelea kutangaza Habari Njema ya Wokovu kama wanavyosimulia Malaika kwa wachungaji waliokuwa Kondeni, usiku ule, watu ambao waliacha yote wakaenda kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Ni matumaini ya Kanisa kwamba, Injili ya Kristo itaendelea kuwaangazia Watu wa Mataifa katika mapito yao, ili kuchuchumilia mwanga na kuachana na matendo ya giza! Kwa njia hii, Wakristo wataendelea kuwa ni mahujaji wa haki na amani, linasema Baraza la Makanisa Ulimwenguni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.All the contents on this site are copyrighted ©.