Padre Gabriel Mmassi, SJ. ni kati ya maelfu ya waamini na mahujaji waliofurika kwenye
Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kusali pamoja na Baba Mtakatifu
Francisko, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 21 Desemba 2014.
Padre Mmassi
anasema, kipindi cha Noeli ni wakati muafaka wa kumfungulia malango ya maisha Yesu
anayezaliwa tena katika mioyo ya watu! Ni wakati wa kuendelea kukesha kwa sala na
tafakari ya Neno la Mungu kama alivyofanya Bikira Maria, kiasi hata akathubutu kukubali
Neno wa Mungu aweze kumwilishwa ndani mwake, na tangu hapo akawa kweli ni Tabernakulo
ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili.
Majilio na hatimaye Kipindi cha Noeli
ni wakati wa kuonjeshana upendo na mshikamano, amani na utulivu, kwani amani ni zawadi
kubwa inayoletwa na Yesu Kriisto Mwana wa Mungu. Waamini na watu wote wenye mapenzi
mema, waendelee kumwombea Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, ili
aendelee kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza Watu wa Mungu kwa njia ya utume
wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Baba Mtakatifu Francisko bado anaendelea
kulihamasisha Kanisa kushikamana na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Haya si mafundisho mapya bali ni mwendelezo wa agizo la Yesu Mwenyewe kwa wafuasi
wake, kama yalivyomwilishwa na Wakristo wa Kanisa la Mwanzo. Kanisa linatambua kwamba,
maskini ni hazina kubwa ya maisha na utume wa Kanisa!